Wanafunzi 1,907 waliopata mimba warejea shuleni

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imesema hadi kufikia Januari, 2023 wanafunzi waliopata ujauzito na kurejea  shuleni kuendelea na masomo ya elimu ya sekondari ni 1,907.

Aidha, imebainisha kuwa wakati wakiendelea na masomo hayo wanafunzi hao wamekuwa wakipatiwa elimu ya makuzi ili kuhakikisha tatizo hilo halijirudii.

Hayo  yamesema leo Juni 28,2023 na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Omary Kipanga bungeni Dodoma wakati akijibu swali la mbunge wa Vitimaalumu Tunza Malapo (Chadema).

Katika swali lake mbunge huyo alitaka kujua Je, ni wanafunzi wangapi wajawazito wamerejea shuleni tangu waraka wa kuwaruhusu utolewe?

Akijibu swali hilo, Kipanga amesema wanafunzi 1,907 wamerejea shuleni na kati yao waliorudi katika Mfumo rasmi ni 562 na waliorejea Nje ya Mfumo Rasmi wa Elimu kupitia Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) ni 1,345.

“Mheshimiwa Spika, kwa upande wa wanafunzi wa Elimu ya Msingi Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Kushirikiana na Ofisi ya Rais- TAMISEMI, inaendelea kukusanya taarifa za wanafunzi waliorejea shuleni baada ya kukatiza masomo kwa sababu mbalimbali,” amesema.

Katika swali la nyongeza la Tunza, alitaka kujua serikali ina mpango gani wa kupungiza muda wa watoto wanaokaa nyumbani pindi wanapomaliza kidato cha nne wakisubiri kujiunga na kidato cha tano.

“Watoto wanakaa hadi miezi nane nyumbani ndio maana kumekuwa na ‘drop out’ nyingi kwa kuwa wanakaa sana nyumbani. Je serikali ina mkakati gani wa kupunguza muda huu,” alihoji.

Akijibu swali hilo, naibu waziri huyo alikiri kuwa wanafunzi wanapomaliza kidato cha nne hukaa nyumbani kwa zaidi ya miezi saba kutokana na shughuli mbalimbali zinazofanywa na serikali kipindi hicho.

Alitaja shughuli hizo kuwa ni usahihishaji na uteuzi wa wanafunzi hao katika shule mbalimbali hali inayochukua muda mrefu.

Hata hivyo, alieleza kuwa ni nia ya serikali kuhakikisha inapunguza muda huo wa wanafunzi kukaa nyumbani ambapo inatarajia kutumia mfumo wa kieletroniki kusahihisha mitihani na uteuzi wa wanafunzi.

“Tayari mfumo wa ‘e marking’ tumeanza kuutumia kwa darasa la saba na sasa tunatarajia kuutumia pia Sekondari,” amesema.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button