Wanafunzi 230,000 Iringa kupewa vyandarua

Wanafunzi 230,000 Iringa kupewa vyandarua

ZAIDI ya wanafunzi 230,000 wa shule za msingi 556 za Mkoa wa Iringa watanufaika na mpango wa serikali wa kugawa chandarua kimoja kwa kila mmoja wao kama sehemu ya mikakati ya serikali ya kutokomeza ugonjwa wa maralia ifikapo mwaka 2030.

Mkakati huo ni mwendelezo wa juhudi za kitaifa na kimataifa kwa kupitia Shirika la Afya Duniani (WHO) zinazolenga kutokomeza maralia katika nchi mbalimbali duniani.

Ugawaji wa vyandarua hivyo unaoratibiwa na Bohari Kuu ya Dawa Tanzania (MSD) umezinduliwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Mhandisi Leonard Masanja katika shule ya msingi Ngome, mjini Iringa.

Advertisement

Meneja wa MSD Kanda ya Nyanda ya Juu Kusini Robert Lugembe alisema kiasi cha Sh Milioni 400 kimetengwa kusambaza vyandarua zaidi ya 230,000 kwa shule hizo mkoani humo.

Wakati wa ugawaji wa vyandarua hivyo, Lugembe alisisitiza kuhusu usalama wake kwa matumizi ya binadamu akisema pamoja na viuatilifu vyake vimetengenezwa hapa hapa nchini.

“Hivyo kwa jamii kuvitumia kwa matumizi sahihi kutasaidia kuondoa kabisa maambukizi ya malaria ifikapo 2030,” alisema.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa alisema inasikitisha kuona baadhi ya familia zikipuuza kwa sababu zozote zile matumizi ya vyandarua pamoja na kuathiriwa na ugonjwa wa maralia mara kwa mara.

“Baadhi ya familia wamekuwa wakitumia vyandarua kukinga mboga mboga zisiharibiwe na wanyama kama kuku huku wengine wakitumia katika shughuli za uvuvi, kinyume na malengo yake na wakati huo huo baadhi ya wnafamilia wakiugua ugonjwa huo,” alisema.

Mhandisi Masanja aliwataka walimu pamoja na wataalamu wa afya mkoani humo kutoa elimu na kusisitiza matumizi sahihi ya vyandarua hivyo, ili kuwezesha malengo ya Taifa na dunia katika kutokomeza ugonjwa huo yafanikiwe.

Aidha Mhandisi Masanja alisema wataanza kuwachukulia hatua za kisheria wananchi watakaovitumia vyandarua hivyo kinyume na malengo yake.

Akizungumza kwa niaba ya wazazi Angel Kisika ameishukuru serikali kwa jitihada na kuwahimiza wazazi na walezi wenzake kuhakikisha wanatumia vyandarua hivyo kila wakati ili kutimiza azma ya serikali ya kukabiliana na ugonjwa huo.

Mpango wa kugawa vyandarua kwa wanafunzi hao umekuja huku mkoa wa Iringa ukiwa umenufaika na programu kama hiyo mwaka 2020 iliyowezesha vyandarua 712,615 kugaiwa kwa wakazi wa mkoa wa Iringa.