Serikali yazindua kitabu safari ya upandikizaji wa moyo 

DAR ES SALAAM: Katika jitihada za kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma za kibingwa bobezi nchini, Serikali imezindua kitabu cha safari ya upandikizaji wa moyo kitakachosaidia kutoa mwongozo na uelewa kwa wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitabu hicho jijini Dar es Salaam, Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan inaendelea kuimarisha sekta ya afya kwa kuwekeza katika huduma za kibingwa na bobezi, ikiwemo matibabu ya magonjwa ya moyo.

Mchengerwa aliipongeza Jakaya Kikwete Cardiac Institute (JKCI) kwa hatua hiyo muhimu, akieleza kuwa mpango huo unaashiria mafanikio makubwa katika utoaji wa huduma za moyo katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.
“Huduma ya upandikizaji wa moyo ni hatua kubwa kwa taifa.

Sasa ni wakati wa kuendelea kuweka miundombinu bora, mifumo imara ya kisheria pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa ili kufanikisha huduma hii,” amesema Mchengerwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Upandikizaji wa Moyo nchini kutoka JKCI, Dkt. Everist Nyawawa, alisema takribani watu milioni 64 duniani wana matatizo ya moyo yanayoweza kuhitaji huduma ya upandikizaji wa moyo ili kuendelea kuishi.

Dkt. Nyawawa, ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji wa moyo, alisema huduma hiyo ni hatua ya mwisho ya matibabu kwa wagonjwa wenye ugonjwa wa moyo kushindwa kufanya kazi (heart failure), ambao mara nyingi hulazimika kutumia dawa na kupata matibabu ya muda mrefu.

Amesema JKCI imeamua kuthubutu kufanya mambo ambayo hapo awali yalionekana magumu ili kuokoa maisha ya Watanzania wengi zaidi.

“Hatua hii muhimu italisaidia taifa
kupunguza gharama za kuwapeleka wagonjwa wanaohitaji kupandikizwa moyo nje ya nchi na kuongeza upatikanaji wa huduma hizi hapa nchini,” alisema Dkt. Nyawawa.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kutoa elimu kwa jamii kuhusu huduma za upandikizaji wa moyo pamoja na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zitakazowekwa ili kufanikisha utekelezaji wake.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Afya amezindua rasmi Bodi ya Wadhamini ya JKCI na kuitaka kuimarisha utawala bora, uwajibikaji na usimamizi wa taasisi hiyo ili kuhakikisha malengo na mikakati iliyowekwa inatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button