Wanafunzi 3,000 kudahiliwa IFM Chato

TAKRIBANI wanafunzi 3,000 wanatarajiwa kunufaika na udahili wa mara ya kwanza wa Chuo cha Usmamizi wa Fedha (IFM) kampasi ya Geita kinachojengwa mtaa mtaa wa Mlimani kata ya Muungano wilayani Chato.

Mkufunzi wa Chuo Cha IFM, profesa Josephat Lotto amesema hayo wakati akitoa taarifa ya mradi kwa kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa aliyefika kukagua na kuweka jiwe la msingi kwenye mradi huo.

Advertisement

Profesa Lotto amesema, huo ni mwendelezo wa kusogeza fursa ya huduma ya elimu ya vyuo vya kati kwa mkoa wa Geita na mikoa jirani na kutengeneza mzingira ya biashara na kujiajiri kwa vijana wa kitanzania.

SOMA: IFM Mwanza wachangia damu

Amesema ili kukamilisha mradi huo takribani kiasi cha Sh 9.7 kimepangwa kutumika kujenga jengo la madarasa lenye thamani ya Sh milioni 476, jengo la utawala Sh bilioni 1.2, jengo la mihadhara sh milioni 797.

Amesema jengo la chakula sh milioni 226.5, mabweni ya wanafunzu Sh bilioni 3.5, nyumba za wafanyakazi Sh milioni 548, jengo la maktaba na tehama Sh milioni 764.

Ameeleza pia mpaka sasa gharama za awali zimetumika kiasi cha sh milioni 332 huku gharama za miundombinu ya maji, umeme, barabara zimegharimu Sh bilioni 1.88.

“Ujenzi wa Chuo hiki ulianza mwezi Januari 2021 kwa matayarisho ya awali, ujenzi wa majengo wa awamu ya kwanza ulianza Juni 2021, Ujenzi wa awamu ya pili ulianza Juni 2022,” amesema Profesa Lotto.

Mbunge wa Jimbo la Chato, Dk Medard Kalemani amesema eneo la hekari 32 linatumika kujenga chuo hicho ambapo maeneo hayo yalikuwa yanamilikiwa na wananchi ambao walilipwa fidia kupisha mradi huo wenye tija.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Godfrey Mnzava ameagiza usimamizi uimarishwe kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kama ilivyopangwa.