Wanafunzi mbaroni kwa udhalilishaji mtandaoni

JESHI la Polisi mkoani Arusha, limefanikiwa kuwakamata wanafunzi wawili wa chuo cha Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru kwa tuhuma za unyanyasaji wa kijinsia kwa mwanafunzi wa chuo hicho kwa njia ya mtandao.

Akitoa taarifa hiyo leo Januari 29, 2023 Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Justine Masejo amewataja waliokamtwa kuwa ni Efron Isaya (32) na Cosmas Robert (26), wote wanafunzi wa mwaka wa tatu katika chuo hicho.

Amesema Januari 21 mwaka huu saa 11 jioni katika Chuo cha Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru (CDTI),  kilichopo Wilaya ya Arumeru kuliripotiwa tukio la unyanyasaji wa kijinsia mwanafunzi wa chuo hicho,  (jina limehifadhiwa) kwa njia ya mtandao na wanafunzi wenzake.

ACP Masejo amesema baada ya kupata taarifa hiyo jeshi hilo lilianza uchunguzi kuhusiana na tukio hilo na kufanikiwa kuwakamata wanafunzi hao wawili.

Masejo amesema bado jeshi hilo linaendelea na upelelezi wa tukio hilo na mara utakapokamilika jalada litapelekwa ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa hatua zaidi za kisheria.

Habari Zifananazo

Back to top button