Wanafunzi wanne waliopata mimba warudi darasani

WANAFUNZI wanne kati ya 19 waliopata ujauzito wakiwa shuleni katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wamerejea kuendelea na masomo yao baada ya kujifungua.

Kurejea kwao shuleni ni utekelezaji wa mwongozo wa kuwarejesha shuleni wanafunzi waliokatiza masomo katika elimu ya msingi na sekondari kutokana na sababu mbalimbali, ambao ulitolewa Februari mwaka jana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Mwongozo huo unatekeleza tamko la kisera la serikali lililotolewa Novemba 2021 kuwaruhusu wanafunzi waliopata ujauzito kurejea katika mfumo wa elimu rasmi baada ya kujifungua.

Ofisa Elimu wa Sekondari katika Halmashauri ya Moshi, Benedict Sandy aliliambia HabariLEO kuwa wanafunzi waliorejeshwa shuleni kuendelea na masomo ni wale walioacha shule mwaka jana na mwaka juzi, wamerudi shuleni mwaka huu kuendelea na masomo yao.

“Wanafunzi waliorudi shuleni mwaka huu, wawili wapo kidato cha tatu na hao wengine wawili ni wa kidato cha nne na wanasoma katika shule za sekondari za Darajani, Mruwia, Cyril Chami na Uparo,” alisema.

“Kidato cha kwanza alikuwapo mwanafunzi mmoja wa shule ya Komakya aliyepata ujeuzito, kidato cha pili mmoja wa Shule ya Lyakirimu, kidato cha tatu wanafunzi tisa kutoka shule za Kimochi, Kirima, Manushi Day, Masoka, Mbokomu, Mpirani, Kilimani, Ghona na Rukima na kidato cha nne ni katika shule za Mboni, Kisuluni, Mruwia, Mangi Marealle, Mashingia, Sakayo Mosha na Uparo na Kidato cha Sita ni Weruweru,” alisema.

Mwongozo wa kuwarejesha shuleni wanafunzi walioacha shule kwa sababu mbalimbali, unatoa hadi miaka miwili ya kurejea shuleni kwa mwanafunzi aliyekatiza masomo kutokana na ujauzito, ukitoa fursa muhusika kumlea mtoto katika miezi yake ya awali ya makuzi.

Kabla ya kumrejesha mwanafunzi, mwongozo unataka uongozi wa shule kuitisha kikao cha pamoja baina ya mzazi ama mlezi na kamati ama bodi ya shule kujadili namna ya kumsaidia mwanafunzi husika. Pia unaelekeza mwanafunzi kurejea shuleni mwanzo wa mwaka mpya wa masomo katika darasa alilokatiza masomo.

“Kupewa huduma ya ushauri unasihi, hairuhusiwi kwa mwanafunzi aliyerejea shuleni baada ya kujifungua kwenda shuleni na mtoto wake,” unaeleza muongozo huo. Kadhalika mwongozo huo unaeleza kuwa unatoa wajibu kwa Ofisa Elimu Msingi ama Sekondari kutoa elimu kuhusu urejeshwaji wa wanafunzi waliokatiza masomo, suala ambalo Sandy alisema baada ya kupata mwongozo huo Februari waliwaita wakuu wa shule na maofisa elimu kata kuwapa elimu husika.

Alisema muongozo ulieleza wazi kwamba mwanafunzi anaweza akarudi kwenye shule ile ile aliyokua akisoma awali au akaamua kwenda kwenye shule nyingine atakayopenda au itakayoamuliwa na wazazi au walezi kwa kushauriana na na yeye mwenyewe.

“Kwa hiyo wanafunzi wanapotaka kurudi shuleni asilimia kubwa wamekuwa wakiomba wabadilishiwe shule. Kwamba alikuwa anasoma Sekondari ya Darajani, sasa anataka apelekwe labda Sekondari ya Marangu,” alisema

Habari Zifananazo

Back to top button