Wanafunzi wapewa sare za shule bure

WANAFUNZI 60 wa Shule ya Msingi Mloganzila A na B wenye uhitaji wamepewa msaada wa sure za shule na watumishi wanawake wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam  baada ya kupokea sare hizo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mloganzila A, Jackson Massasi amewashukuru watumishi hao pamoja na uongozi wa hospitali ya Mloganzila kwa msaada huo na kuwaomba wawakumbuke tena wakati mwingine kwa sababu wanafunzi bado wana uhitaji.

“Mungu awabariki kwa msaada huu mliotoa kwa wanafunzi hawa, mmewagusa kwa kiasi kikubwa na siku zote wataendelea kuwakumbuka kila watakapokuwa wanavaa sare hizi,” amesema  Massasi.

Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila Dk Julieth Magandi amewapongeza watumishi hao kwa msaada waliotoa kwa wanafunzi hao ambao ni taifa la kesho.

“Matendo ya huruma ya namna hii ni kama ibada yenye baraka, hivyo matendo haya yasiishie kwenye kutoa sare za shule tu, nawaomba muendelee kujipanga kwa kadri mtakavyojaliwa ili kugusa jamii kwa upana zaidi,” amesema Dk Magandi.

Dk Magandi ameongeza kuwa MNH-Mloganzila iliwahi kutoa msaada katika shule hiyo ambapo iliwajengea matundu matano ya vyoo, ambavyo viligharimu kiasi cha Sh Milioni 15 na pia ilimtafuta mfadhili ambaye alitoa msaada wa kujenga matundu mengine matano na kufikisha idadi ya matundu 10.

Habari Zifananazo

Back to top button