WANANCHI 300 kutoka wilayani Kahama mkoani Shinyanga wamefanyiwa uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi, matiti na tezi dume huku wataalamu wakitoa ushauri kuwa viashiria vya saratani vikiwahiwa mapema vinatibiwa.
Meneja wa Huduma za Uchunguzi wa Saratani na Elimu kwa Umma kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dk Maguha Stephano amesema hayo leo katika zoezi la uchunguzi, matibabu na elimu iliyodhaminiwa na Benki ya NBC.
Dk Stephano amesema lengo kwa wilaya hii ni kuwafanyia uchunguzi zaidi ya wananchi 1000 na wanatibiwa bure na madaktari bingwa wa saratani kutoka Ocean Road ambapo benki hiyo iliamua kila senti kuipeleka katika huduma ya matibabu.
Dk Stephano amesema Saratani ya Mlango wa kizazi wanawake 160 walifanyiwa vipimo na wawili walibainika kuwa na viashiria na walipatiwa rufaa ya kwenda Hospitali ya Ocean Road na wengine wawili watafanyiwa upasuaji kwani Saratani ukiiwahi kwa kuona viashiria vya mwanzo inatibiwa.
“Kuna Wanaume 57 wenye kuanzia umri wa miaka 50 na kuendelea wamefanyiwa uchunguzi wa tezi dume ambapo Wanaume wawili walibainika kuwa na viashiria vya ugonjwa huo” amesema Dk Stephano
Meneja kutoka Benki ya NBC tawi la Kahama, Saimon Ntwale amesema kupitia NBC Marathon Dodoma wametoa elimu juu ya madhara ya saratani na wameingia ubia wa kuchangia matibabu na kufanya uchunguzi.
“Matibabu na uchunguzi vina gharama kubwa na huu no msimu wa tano kwa kutoa huduma hii nchini kwa kuwafikia wanawake zaidi ya 40,000 kwa vipimo na matibabu bure kwa wananchi,”amesema. Ntwale.
Mmoja wa wanawake walifanyiwa uchunguzi kutoka Manispaa Kahama Winfrida Salvatory amesema amefanyiwa uchunguzi wa saratani ya matiti bure huku akiwashauri wanawake wajitokeze kufanyiwa uchunguzi ili wajue afya zao.