WANANCHI wanaoishi Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara wenye sifa za kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa wamehimizwa kuchukuwa fomu za kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi utakofanyika Novemba 27, 2024.
Fomu za kugombea zinapatikana katika ofisi ya msimamizi msaidizi wa uchunguzi kwenye manispaa hiyo.
Akizungumza leo Septemba 26, wakati akitoa maelekezo kwa viongozi kutoka taasisi mbalimbali za manispaa hiyo kuhusu uchaguzi huo, msimamizi wa uchaguzi katika manispaa hiyo, mwalimu Hassan Nyange ametaja kigezo kuwa ni kwa wenye umri kuanzia miaka 21.
Aidha fomu za kugombea nafasi hizo zitatolewa na kurejeshwa kuanzia Novemba 1 hadi Novemba 7,2024 kwa msimamizi msaidizi wa uchaguzi katika manispaa hiyo.
Hata hivyo zoezi la uandikishaji wapiga kura litafanyaika kuanzia Oktoba 11 hadi Oktoba 20, katika vituo vilivyopwangwa huku wakazi wenye sifa za kupiga kura wenye umri wa kuanzia miaka 18 au zaidi na wale wanaokidhi masharti ya kisheria wamehimizwa kushiriki katika uchaguzi huo.
‘’Maelekezo haya yanalenga kutoa mwongozo ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uwazi, haki na usawa kwa kuzingiatia sheria na taratibu zilizowekwa na kuhakikisha taratibu zote zinafatwa na kwamba wapiga kura pamoja na wagombea wanapata taarifa zote zinazohitajika kwa wakati,’’amesema Nyange.
SOMA:TPDC yaja kivingine upatikanaji gesi
Baadhi ya viongozi hao akiwemo Shamsa Yusufu mkazi wa kata ya majengo kwenye manispaa hiyo amesema “Nimejiandaa vizuri kushiriki katika uchaguzi huu na waambia wananchi wajitikeze kwa wingi kupiga kura ili kumchagua kiongozi aliyekuwa bora.”
Hata hivyo baadhi ya viongozi wa dini akiwemo Shekhe Hassan Mpwago kutoka Baraza Kuu la Waislamu (BAKWATA) mkoani humo amesema “Mpaka sasa uchaguzi utakuwa ni mzuri kwasababu tuna imani na tunachoomba sisi yale yaliyopo katika mwongozo yafanyike vizuri.”