TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Morogoro imewaomba wananchi waliojiandikisha kushiriki kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa kujitokeza kwa wingi kupiga kura Novemba 27, 2024 na kuchagua viongozi waadilifu ili kuleta maendeleo katika maeneo yao .
Mkuu wa Takukuru mkoa huo, Pilly Mwakasege amesema hayo Novemba 26, 2024 wakati akitoa taarifa kwa umma ya robo mwaka ya Julai hadi Septemba 2024 kupitia waandishi wa habari mkoani Morogoro.
Mwakasege amewaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa Takukuru na taarifa za vitendo vya Rushwa na kuwa tayari kutoa ushahidi ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria .
Amesema,Takukuru inaendelea kutoa elimu ya mapambano dhidi ya rushwa kwa wananchi ,vyombo vya habari na vyama vya siasa ili waweze kushiriki kikamilifu katika udhibiti wa vitendo vya rushwa hasa kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaofanyika leo Novemba 27, 2024.
Amesema Takukuru kupitia kitengo cha intelejenjia kimekuwa kimekuwa kikikusanya na kupokea taarifa za vitendo vya Rushwa mapema kabla ya hata kuanza kwa uchaguzi .
“Kwa sasa hatuwezi kutoa takwimu za idadi ya taarifa zilizotufikia kwani leo ( jana ) tunatoa taarifa ya robo mwaka ya Julai hadi Septemba 2024,” amesema Mwakasege.
Mwakasege amesema Takukuru inakusanya taarifa za viashiria vya rushwa katika uchaguzi na kuzifanyia kazi licha ya kwamba nyingine si za kiuchunguzi moja kwa moja,lakini zimekuwa zikifuatiliwa kwa karibu zaidi ili kuzuia vitendo vya rushwa.
“ Hapa leo sina idadi ya taarifa ila tunazipokea kwa wingi na zikipokelewa zinafanyiwa uchambuzi na zikifanyiwa uchambuzi kuna zile za kufanya udhibiti kwa kufuatilia maeneo husika ili kubaini ukweli wake na kama upo ukweli hatua zinachukuliwa mara moja ” almesema Mwakasege.
Mkuu wa Takukuru wa mkoa amesema kuwa endapo yatatokea malalamiko ambayo yana ushahidi ,hatua za kisheria zitachukuliwa kwa maana ya uchunguzi na wahusika kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria .
“ Lakini kwa sasa taarifa tunazo na bado zinaendelea kufanyiwa mchakato na bado tunaendelea kupokea taarifa na tuna watu wapo huko kazini ( mitaani),“ amsema Mwakasege.