WANANCHI katika Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara wamehimizwa kujitokeza kupata matibabu ya magonjwa mbalimbali yanayohitaji kuonana na madaktari bingwa na wabobezi yanayofanyika wilayani humo kuanzia Novemba 19 hadi 21, 2024.
Timu ya madaktari bingwa na wabobezi wa afya ya binadamu mkoani humo wameandika historia kwa kuanza kutoa kliniki ya kwanza ndani ya mkoa ya magonjwa mbalimbali kutokana na kuwepo kwa vifaa tiba vya kutosha.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amebainisha kuwa madaktari bingwa na wabobezi 15 watatoa huduma kwa kuweka kambi katika wilaya moja ili wananchi wote wanaohitaji huduma ya kibingwa na kibobezi waweze kupata tiba kutokea kwenye eneo hilo kabla ya kuhamia katika wilaya zingine
“Hii ni fursa ndugu zangu wananchi inapunguza gharama za kusafiri kwenda kufuata huduma za kibingwa na kibobezi katika mikoa mingine pamoja na gharama za kuwaona madaktari bingwa hao,”amesema Sendiga.
Hatua hiyo inaunga mkono wazo lililobuniwa na Rais Samia Suluhu Hassan la kuwapatia wananchi wote huduma za kibingwa na bobezi katika kufikia malengo ya mpango mkakati wa taifa wa afya kwa wote ifikapo mwaka 2030.
Kwa kujibu wake mpango huo unasaidia kufanya uchunguzi wa wali wa magonjwa mbalimbali kabla ya kuwa sugu, kuwajengea uwezo watumishi wa afya kupitia madaktari bingwa na wabobezi wa mkoa pamoja na kufahamu uhalisia wa magonjwa katika eneo husika.
“Kwa kuwa vifaa tiba tunavyo na madaktari bingwa na wabobezi tunao ambao watatoa huduma endelevu tumeona hakuna sababu ya kuendeleza.kusubiri ratiba ya madaktari bingwa na wabobezi ya kitaifa wapite sisi tunaanza na madaktari bingwa tulionao ndani ya mkoa kuunga juhudi za Rais Dokta Samia Suluhu Hassan,” amesema Sendiga.
Magonjwa yanayoshughulikiwa ni ya upasuaji,dawa za usingizi, wanawake na watoto na masuala ya uzazi.Magonjwa mengine ni shinikizo la damu,kisukari, magonjwa ya moyo,macho na mengineyo.
Sambamba na hilo anafafanua kubwa hakutakuwa na gharama za kuwaona madaktari hao za nyongeza bali ni gharama.zilizoelekezwa na serikali za kumuona daktari bingwa yoyote.
Kwa upande wake Mganga Mkuu Mkoa wa Manyara, Andrew Method anawahimiza wanawake kuhudhuria kliniki kupata ushauri wa madaktari ili kujiepusha na magonjwa yanayopelekea vifo vya wajawazito ikiwemo kifafa cha mimba.