WANANCHI wa kata ya Mlimani na Boma zilizopo Manispaa ya Morogoro wamesema wataendelea kuwa walinzi wazuri katika kudhibiti vitendo vya uchomaji moto misitu ya asili na hifadhi ya milima Uluguru ambayo ni tegemeo kubwa kijamii na kiuchumi.
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeanzisha wiki maalumu ya kampeni ya mapambano dhidi ya moto ikiwa imebeba ujumbe: “Usiazishe moto usiouweza kuuzima kuwa mwenye tahadhari ya moto.”
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwa niaba ya wananchi, wenyeviti wa mitaa ya Kibwe na Mbete walisema mitaa yao wameunda kamati za mazingira zinazowashirikisha vijana zenye jukumu la udhibiti wa moto na ufuatiliaji kwa wanaoandaa mshamba kwa kuchoma moto majani.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kibwe, Kata ya Boma, Thobias Augostino amesema kumekuwa na ushirikiano na wenzao wa mitaa ya kata ya Mlimani kwenye suala la kuzuia viashiria vyoyote na watu kutumia moto pasipo kutoa taarifa katika kamati zao ili tahadhari ziweze kuchukuliwa.
“ Tunazo sheria ndogo za mazingira na endapo mtu akivunja sheria anaadhibiwa kulingana na makosa yaliyotendeka,“ Thobias amesema.
SOMA: Samia aonya uchomaji misitu
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbete, Kata ya Mlimani, Feruzi Mohamed Feruzi amesema wapo mstari wa mbele kutunza mazingira na kwa miaka mingi hakuna matukio ya uanzishawaji wa moto.
Amesema Kamati ya Mazingira ipo makini kudhibiti moto na ufuatiliaji wananchi wanapoandaa mashamba na zinachukua jukumu la kuwashauri wananchi kuchukua tahadhari ya moto uziweze kuleta madhara katika misitu ya asili na na hifadhi.
Naye Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Mbete ,Jonson Mremi amesema kuwa wamekuwa na vipindi vya elimu ya mazingira kwa wanafunzi wa shule hiyo ili kuwarithisha urithi wa malisimali za mali asili kwa ajili ya manufaa yao ya baadaye.
SOMA: Askari wa misitu wasio na maadili kukiona
Mwalimu Mremi amesema licha ya vipindi vya elimu ya mazingira, shule hiyo ina kitalu cha miche ya miti kwa ajili ya kupanda kuzunguma eneo la shule na majirani ikiwa na kuwaelekeza wanafunzi kutambua elimu ya mazingira na kupinga vita vitendo vya uharibifu na uchomaji moto misitu.
Naye Mhifadhi wa TFS , Shaaban Kiulah kutoka Kanda ya Mashariki amewakumbusha wananchi wa kata hizo na nyingine kutambua jukumu la utunzaji wa mazingira na misitu si la serikali pekee bali pia ni jukumu la jamii mzima.
Kiulah amesema ni vyema kila mwananchi kuwa na uchungu kulinda na kuisimamia rasilimali ya misitu, kutii sheria bila shuruti na kuchukia pale moto unapojitokeza ndani misitu ya asili nay a uhifadhi.
“Endapo uharibifu huo unaotokana na uchomaji moto unachangia kuleta madhara makubwa kwa viumbe hai wengine na kusababisha ukosefu wa mvua zisizotabirika na vyanzo vya maji kukauka,“amesema Kiulah.
Mara nyingi chanzo cha moto katika milima ya Uluguru inachangiwa na baadhi ya wananchi kufanya shughuli za kibinadamu zikiwemo za kuandaa mashamba kwa kutumia moto na uchomaji mkaa.
Comments are closed.