Waombwa kuwaunga mkono wahitimu VETA Kongwa

WITO umetolewa kwa wananchi kushiriki katika kutangaza na kutumia bidhaa zinazozalishwa na wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) ili waweze kuwaunga mkono na kuthamini mafunzo yanayotolewa. Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, Fortunatus Mabula amesema hayo katika mahafali ya tatu ya wahitimu 80 wa ngazi ya pili katika fani mbalimbali wa Chuo cha VETA Kongwa.

Mabula amesema chuo hicho kipo kwa ajili ya kusaidia jamii moja kwa moja hivyo jamii itumie bidhaa kama matofali, huduma ya matengenezo ya magari na ushonaji nguo zinazozalishwa na wanafunzi hao ili kuwaunga mkono. “Jamii ihamasike kutumia bidhaa zinazozalishwa kwani ni bora na njia hiyo itawahamasisha vijana wengi zaidi kujiunga na vyuo vya ufundi na hatimaye waweze kujiajiri au kuajiriwa,” alisema.

Katika mahafali hayo mgeni rasmi alipata wasaa wa kutembelea karakana za ushonaji, magari, umeme na kiwanda cha kufyatua matofali ambapo alisisitiza uongozi wa Chuo cha VETA Kongwa kutangaza kazi wanazozifanya ili jamii iweze kuwaunga mkono kwa kutumia bidhaa zao. SOMA: Bil 19.1/- zatumika kujenga vyuo vya VETA 4

Mabula alitoa msisitizo kwa wazazi kutumia Chuo cha VETA kuwapeleka watoto kupata ujuzi na kuepuka kukaa nyumbani na watoto wasiokuwa na shughuli za kufanya. Aidha, aliwasihi wahitimu wazingatie maadili na kutumia vizuri ujuzi walioupata ili kuwainua kiuchumi na kusaidia taifa kwa ujumla kwani elimu ya VETA ni ujasiriamali wa moja kwa moja.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa chuo cha VETA Kongwa, John Magulyati alisema kuwa ili kuhakikisha hakuna Mtanzania anayekosa elimu kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo wanafunzi waliokatisha masomo kutokana na kupata ujauzito, chuo kimeanza kutoa kozi za muda mfupi kwa mabinti wanaonyonyesha watoto wenye umri kuanzia miezi mitatu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button