Wananchi wasaidiwe kujua mifumo kudhibiti matumizi ya data

KATIKA siku za hivi karibuni Watanzania watumiaji wa huduma za intaneti wamekuwa wakishutumu watoa huduma za mawasiliano ya simu za mkononi kwa kupandisha gharama za vifurushi kumalizika haraka kabla ya muda.

Watanzania hao walisajili malalamiko yao kwenye ukurasa wa mtandao wa Twitter wa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ambaye aliamua kulivalia njuga kwa kuweka juhudi katika kuwaelewesha mwenendo mzima wa gharama za kusafirisha data.

Nape kupitia ukurasa wake na baadaye kipindi cha 360 cha Kituo cha Televisheni cha Clouds alieleza namna serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inavyofanya juhudi za kudhibiti gharama za kusafirisha data ili watoa huduma wasivuke viwango elekezi vilivyowekwa na mamlaka. Nape ameweka wazi kuwa katika kudhibiti gharama hizo Tanzania imekuwa ni moja ya nchi zilizo katika orodha ya nchi zenye gharama za chini za viwango vya kusafirisha data.

Pia ameeleza kuhusu tatizo la vifurushi kuisha haraka linalotokana na baadhi ya watumiaji kutokujua matumizi sahihi ya simu. Maelezo ya Nape yamenifanya nigundue kwamba hata mimi ni mmoja kati ya waliokuwa wakihisi kuibiwa vifurushi kumbe hali ile inatokana na matumizi yasiyo sahihi ya aplikesheni ndani ya data za intaneti.

Hapo naona umuhimu wa mamlaka husika au watoa huduma kuweka utaratibu maalumu wa kuwaelewesha wateja wao matumizi sahihi ya intaneti ili kupunguza malalamiko na lawama dhidi yao.

Sambamba na hilo watumiaji wenyewe wa mitandao ya simu waone namna ya kufanya juhudi za kujifunza matumizi sahihi ya intaneti yatakayowasaidia kupunguza tatizo la vifurushi kuisha haraka.

Habari Zifananazo

Back to top button