Wananchi wataka kituo cha afya Kandaga kikamilike

KIGOMA: Mabalozi na wananchi wa kata ya Kandaga Halmashauri ya Wilaya Uvinza mkoani Kigoma wameiomba serikali kukamilisha mradi wa kituo cha afya katika kata hiyo ili waondokane na shida ya muda mrefu ya kufuata matibabu mbali kwa gharama kubwa.
Wananchi hao wamesema hayo mbele ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Abdulkadri Mushi wakati wa maadhimisho ya kiwilaya ya sherehe za miaka 49 ya kuzaliwa CCM yaliyoenda sambamba na ukaguzi wa miradi uliofanywa na Kamati ya Siasa ya Mkoa Kigoma.

Mmoja wa mabalozi aliyehudhuria maadhimisho hayo yaliyoenda sambamba na kujitolea kufanya kazi katika mradi wa ujenzi wa kituo hicho cha afya, Marystela Kishanga amesema kuwa serikali imetoa fedha na kuahidi mradi huo kuanza kutoa huduma mwezi Aprili mwaka huu hivyo wameomba ahadi hiyo ya serikali itekelezwe.
Akizungumza baada ya kutembelea, kukagua na kushiriki kwenye kazi ya ujenzi wa kituo hicho cha afya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Abdulkadri Mushi amesema kuwa mradi huo haukuja kwa bahati mbaya bali ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.

Mushi alisema kuwa wamesikia kilio cha wananchi kuhusu mradi huo na hivyo ameungana na wananchi hao kutoa maelekezo kwa Mkuu wa Wilaya Uvinza na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Uvinza kusimamia mradi huo kwa viwango na kukamilika kwa wakati ili huduma zianze kutolewa.



