‘Wananchi wengi hawapendi njia ya usuluhishi’

‘Wananchi wengi hawapendi njia ya usuluhishi’

WANANCHI walio wengi hawapendi njia ya usuluhishi  kwa kuamini kuwa kazi ya mahakama ni moja tu ya kufunga watu gerezani, imeelezwa.

Hayo yalibainishwa jana Januari 22, 2023 na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi, Glory Mwakihaba katika uzinduzi wa Wiki ya Sheria uliofanyika kiwilaya katika viwanja vya Shule ya Msingi Mpanda Ndogo, Kijiji cha Majalila Kata ya Tongwe.

Mwakihaba ametumia fursa ya maadhimisho hayo kuwaelimisha wananchi kwamba usuluhishi ni njia bora na rahisi katika utatuzi wa migogoro  duniani kote, ukilinganisha na uendeshaji wa kesi kwa njia ya kawaida.

Advertisement

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi, Glory Mwakihaba akizungumza kwenye uzinduzi huo (Picha zote na Swaum Katambo).

Amesema kesi huchelewa kukamilika na kuchukua muda mrefu,  kwa sababu ya kufuata sheria na taratibu kitendo ambacho kinadumaza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

“Mwananchi atapoteza muda wake mwingi kuhudhuria mahakamani na kukosa muda wa kufanya shughuli za uzalishaji,” amesema.

Hata hivyo amesema kuwa katika wilaya hiyo kwa muda mfupi waliofanya kazi, wamebaini kuwa vitendo vya kujichukulia sheria mkononi, matukio ya ukatili wa kijinsia, mauaji, mimba za utotoni ni matukio yanayoongoza kujirudia mara kwa mara, hivyo watajikita katika kutoa elimu zaidi kwa wananchi.

Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu, akizungumza kwenye uzinduzi huo.

Kwa upande wake mgeni rasmi katika uzinduzi huo Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu, ametoa wito kwa taasisi zote za Serikali ,kutoa ushirikiano wa kutosha, ili mhimili wa Mahakama uweze kutekeleza na kuifikia azma ya kutoa elimu kwa wananchi.

“Wananchi hawa ninyi mnafanya nao kazi, lakini wakati huo wakiwa wamesongwa na migogoro ambayo inawezekana katika nafasi zenu na majukumu yenu hamjafanikiwa kuitatua, lakini kupitia elimu ambayo Mahakama itatoa kwa muda wa juma zima tutapata elimu ya kutusaidia,” amesema Buswelu.

Kwa upande wao wananchi pamoja na baadhi ya viongozi wa kijiji na kata wamesema watatumia fursa ya elimu watakayopatiwa na watendaji wa mahakama wa wilaya hiyo, kupunguza matukio mbalimbali yanavyovunja sheria za nchi yanayoweza kuepukika katika jamii.