Wanane wajeruhiwa happy nation ikipinduka Vigwaza

WATU wanane wamejeruhiwa baada ya basi la Happy Nation lililokuwa likitokea Bukoba kwenda Dar es Salaam kupinduka wakati likijaribu kulipita gari lililokuwa limesimama katika eneo la Ruvu, Vigwaza wilayani Chalinze mkoani Pwani, Kamanda wa Polisi, ACP Pius Lutamo amethibitisha.

ACP Pius Lutumo alisema ajali hiyo ilitokea Machi 2, 2023 saa 8:30 usiku kwenye Kijiji cha Ruvu Kata ya Vigwaza Wilaya ya Kipolisi Chalinze Bagamoyo.

“Basi hilo lenye namba za usajili T 526 DVJ lilikuwa likiendeshwa na Vincent Mbasha (39) mkazi wa Mbezi Jijini Dar es Salaam na chanzo lilikuwa likilikwepa gari la mizigo aina ya Scania lenye namba T 299 BYF na tela namba T 308 BYF lilikuwa limepata hitilafu na kutoweka alama yoyote kuashiria kuwa kuna gari ndipo dereva huyo wa basi akalikwepa na kupinduka,”alisema Lutumo.

Alisema basi hilo lilikuwa na abiri 47 ambapo majeruhi wako hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi kwa matibabu zaidi ambapo hali zao zinaendelea vizuri.

Aidha aliwataja majeruhi hao kuwa ni Nuru Mohamed (38), Selimanda Abdala (63), Amina Jumanne (48), Faudhia Ismail (23), Fredina Omary (15) Abtatus Jovin (18), Idat Reman (27) na Aida Suleiman (24).

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge ambaye aliwatembelea majeruhi hao alisema kuwa madereva wanapaswa kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zisizo za lazima.

Kunenge alisema kuwa alipata taarifa kuwa dereva huyo alitaka kulipita gari hilo upande wa kulia badala ya kushoto ambapo ni uzembe hivyo ni vema wakazingatia sheria.

Mganga Mfawidhi wa Tumbi Amani Malima alisema kuwa waliwapokea majeruhi hao ambapo wameumia maeneo mbalimbali ya miili yao na wanaendelea vizuri na matibabu. Malima alisema kuwa wagonjwa hao wanaendelea na vipimo mbalimbali vikubwa ilikugundua majeruhi hao wameumia kiasi gani.

Habari Zifananazo

Back to top button