Wanane watunukiwa kwa kudumisha Muungano

DODOMA; RAIS Samia Suluhu Hassan amewatunuku nishani ya Kumbukumbu ya Muungano daraja la pili na la tatu kwa viongozi wastaafu, mawaziri na viongozi waandamizi wanane waliokuwa na mchango katika kudumisha, kulinda na kuimarisha muungano wakati wa uongozi wao.
Rais Samia alitunuku nishani hizo katika Maadhimisho ya Miaka 61 ya Muungano, ikulu Chamwino, Dodoma jana.
Waliotunukiwa nishani hizo ni Makamu wa Rais mstaafu, Dk Ali Mohamed Shein, ambaye Rais Samia alisema mchango wake ni katika kutekeleza majukumu ya kisera, kikatiba na kisheria ikiwemo kuratibu masuala ya muungano na mazingira.

Alisema katika masuala ya Muungano, Dk Shein alishiriki kuanzishwa kwa mifuko ya maendeleo ya kiuchumi iliyotekelezwa pande zote za muungano ikiwemo Mkukuta na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Pia, alisema aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Pamoja ya SMZ na SMT kwa ajili ya kushughulikia changamoto za Muungano.
Mwingine aliyetunukiwa ni aliyewahi kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Seif Ali Iddy, aliyehudumu katika nafasi hiyo 2010/2020 ambaye pia aliwahi kuwa Makamu Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar 2000/2002 .
Kwa mujibu wa Rais Samia, Seif akiwa balozi wa Tanzania nchini Uholanzi 1985, aliiwakilisha Tanzania katika Shirika la Kuzuia Silaha za kemikali, mfuko wa pamoja wa bidhaa, mahakama ya kimataifa ya jinai na Mahakama ya Kimataiifa ya haki.
Mwingine ni Waziri Mkuu Mstaafu wa Awamu ya Nne, Edward Lowasa, ambaye nishani yake ilipokewa na mkewe, Regina.
Lowassa alitunukiwa nishani hiyo kutokana na mchango wake katika kulinda na kudumisha muungano akiwa Waziri Mkuu (2005/2008).

Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda alitunukiwa nishani hiyo kwa mchango wake katika kipindi cha uongozi wake akiwa Waziri Mkuu 2008 hadi 2015 alipostaafu na kushika nafasi nyingine.
Wengine ni Spika mstaafu wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Amir Kificho, aliyewahi kuwa Mjumbe wa Tume ya Nyalali (1991/1992) mjumbe wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (1995/2016) na mwangalizi wa kisisasa wa uchaguzi wa Zanzibar 2020.
Rais Samia alimtunuku nishani Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma, ambaye ni Jaji Mkuu wa Mahakama Tanzania kwa sasa na aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria nchini 2007/2012.

Aidha, Rais Samia limtunuku Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, John Kijazi nishani ya muungano kutokana na mchango wake alipokuwa katika wadhifa huo tangu 2016 hadi 2021 alipofariki.
Kwa upande wa aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2012 hadi 2022, Philip Mangula, pia alitunukiwa nishani ya muungano daraja la tatu.



