SERIKALI imesema wananchi wanaojitolea, Polisi na madereva wanaoendesha magari ya ‘ambulance’ wanahitaji kupewa mafunzo namna ya kuhudumia wagonjwa wa dharura ili wasaidie kuokoa maisha ya watu katika majanga mbalimbali.
Hayo yamesemwa Dar es Salaam na Mkuu wa huduma za dharura, kitengo cha dharura na maafa, Wizara ya afya Erasto Sylivanus wakati wa kufunga awamu ya kwanza ya mradi wa kuboresha huduma za dharura (IMECT) ulioendeshwa kwa ushirikiano na Hospital ya Aga Khan na Kituo cha kimataifa cha msaada la Poland (PCMC).
,”Tumeanza kwa vituo vichache Dar es Salaam na Zanzibar lakini ni mahitaji yanayohitajika nchi nzima. Kama serikali inaelewa umuhimu wa huduma za dharura na inaendelea kuimarisha kwa kipindi kirefu,”amesema.
Amesema katika kipindi cha miaka miwili ya mradi huo serikali imefanya upanuzi wa huduma kwa kujenga na kuweka vifaa kwa idara za dharura mpya kutoka saba zilizokuwepo 2021 hadi sasa ni 121.
Amesema sehemu kubwa iliyobaki ni mafunzo, wataalam wawe wanafundishwa kwa muda mfupi na kurudi kutoa huduma ambazo wananchi wanazihitaji.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Momahed Mang’una amesema mradi huo umesaidia kwasababu umeweza kutoa mafunzo ya aina mbalimbali kama ya huduma za uokoaji kwa walimu na Polisi.
“Tumepata vifaa vinavyosaidia uokozi na namna ya kuzidi huduma za dharura. Tumepata kituo ambacho wanaweza kupata mafunzo namna ya kufanya huduma za dharura,”amesema.
Amesema bado uhitaji upo wanaendelea na mazungumzo na Poland kuhusu uwezekano wa kuendelea nao ili kuwa na mwendelezo wa mafunzo.
Mtendaji Mkuu wa PCMC Wojtek Wilk amesema kupitia mradi huo uliogharimu sh bilioni 1.8 umewanufaisha zaidi ya watu 2000 kupitia mafunzo mbalimbali.
Amesema wao wamejiandaa kuendelea kushirikiana na serikali na sekta binafsi kutoa mafunzo kwa wahudumu ili waweze kufanya kazi hiyo kwa ufanisi.
Daktari bingwa wa magonjwa ya dharura wa Hospitali ya Aga Khan Dk Hussein Manji amesema lengo kuu la mradi ilikuwa ni kuwawezesha watanzania kupata huduma bora ya dharura.
“Tunaishukuru serikali chini Rais Samia Suluhu Hassan kwasababu tunaenda pamoja na serikali katika kutimiza malengo yake katika kudumisha huduma za dharaura, tunashukuru pia, serikali ya Poland kwa kutusapoti,”amesema.