DAR ES SALAAM; KUELEKEA Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu,viongozi wa dini wametoa wito kwa wanasiasa na viongozi wa serikali kuheshimu makubaliano ya maridhiano ya kisiasa, ikiwa ni pamoja na kuheshimu sheria zilizopo wakati wa mchakato wa kutafuta katiba mpya ukiendelea.
Wametoa wito huo leo wakati wa mkutano wa kitaifa wa wadau kujadili hali ya demokrasia nchini kuelekea Uchaguzi Serikali za Mitaa ,Vijiji na Vitongoji mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025 ulioandaliwa na kituo cha demokrasia Tanzania TCD.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania, Mchungaji Canon Moses Matonya, amesema ni vyema katika kuelekea uchaguzi kuwepo na utashi kwa viongozi wote na kuweka mazingira mazuri kwa chaguzi zijazo, huku akiwasihi kuienzi demokrasia iliyowekwa na waasisi wa Taifa la Tanzania.
Kwa upande wake Amiri Mkuu wa Baraza la Kiislamu Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Shehe Mussa Kundecha, amewasihi viongozi hao kuwa na makubaliano miongoni mwao na kuyaheshimu, kwani jambo hilo litawasaidia hata viongozi wa dini kuwahimiza waumini kuwaheshimu.
Akieleza demokrasia iliyopo nchini Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana, amesema demokrasia imekua sana nchini kutokana kuwepo kwa wabunge mbalimbali wa vyama tofauti kushiriki katika vikao vya bunge, huku akikiri kuwa yapo mapungufu katika kusimamia sheria na kuhakikisha umma kuwa uchaguzi ujao utakuwa wa haki na huru.
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika, Mwenyekiti wa chama cha ACT Wazalendo, Juma Duni wakitoa maoni juu ya kuleta amani ya uchaguzi huo wamependekeza mchakato wa kuanza kubadilisha katiba mpya kuanza mara moja na sheria zipelekwe bungeni, ili ziwape nafasi kufanya uchaguzi wa haki.
Comments are closed.