WANAUME wawili wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wakiwa wamevalia gauni na vilemba kwa lengo la kuficha utambulisho wao, wameuawa kwa kupigwa risasi na askari polisi baada ya kumvamia mfanyabiashara, Flora Abdallah (42) mkazi wa Mtaa wa Kabambo Kiseke, Ilemela, Mwanza.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa alisema tukio hilo lilitokea Julai 9, 2024 saa 2.45 usiku.
Alisema wanaume hao walivamia nyumba ya mfanyabiashara huyo wakitaka kufanya uhalifu, wakiwa na bunduki aina ya shortgun na panga mbili.
Alisema walikutana na askari polisi waliokuwa kwenye doria, ambao waliwaamuru wajisalimishe, lakini walikataa na kujaribu kuwadhuru askari na wakazi wa eneo hilo. Hivyo, askari walifyatua risasi, na watu wawili walijeruhiwa na kufa papohapo.
Alisema miili yao imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa uchunguzi na utambuzi.
Mutafungwa alisema hakuna mali iliyoibwa katika tukio hilo. Silaha na vifaa vingine pamoja na watu wawili waliokimbia kwa pikipiki, vimepatikana.
Katika tukio lingine, Mutafungwa alieleza ajali ya gari ilitokea Januari 10, 2025 asubuhi katika eneo la Iseni, Butimba, Nyamagana.
Alisema ajali hiyo ilihusisha gari aina ya Toyota Coaster iliyogonga gari aina ya Toyota IST na kuathiri gari nyingine aina ya Toyota Hiace.
Alisema katika ajali hiyo mwanamke wa miaka kati ya 20-25 alifariki na watu wanne walijeruhiwa.