Wanavyuo watakiwa kujitokeza uchaguzi mitaa

KUELEKEA uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27,2024, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara, Abdallah Mwaipaya amewataka wanavyuo wote na wanafunzi waliotimiza umri wa miaka 18 na kuendelea kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwenye uchaguzi huo.

Akizungumza kwenye Mtwara Samia Uni Bonanza, mkuu huyo wa wilaya amesema lengo la bonanza hilo ni kuhamasisha vijana hasa wanavyuo kuhusu haki zao za kiraia na kutoa fursa ya kujifunza kuhusu mchakato wa uchaguzi na mchango wa elimu katika maendeleo ya taifa.

Bonanza hilo limefanyika leo Novemba 23,2024 katika viwanja vya Nangwanda Sijaona mkoani humo na kuandaliwa na ofisi ya mkuu huyo wa wilaya.

Advertisement

“Ili demokrasia iendelezwe ni muhimu wanafunzi hawa washiriki kwenye uchaguzi na kuchagua viongozi bora watakao paza sauti za vijana  na kuwashirikisha katika maendeleo ya sehemu husika”amesema Mwaipaya

Amesisitiza suala la kutumia fursa ya uchaguzi wa Serikali Za Mitaa kama sehemu ya kuonyesha uongozi na ushiriki wao katika mambo mbalimbali ya kijamii.

Msimamizi wa uchaguzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani Hassan Nyange ametoa wito kwa wanafunzi hao kujitokeza mapema kwenda kupiga kura na kurudi nyumbani kusubiri matokeo.

Baadhi ya wanafunzi hao akiwemo Fatuma Ally “Tumejiandaa vizuri kushiriki uchaguzi huu na kuchagua kiongozi atakae kuwa chachu ya kuleta maendeleo kwenye maeneo yetu na mwenye kuchochea ustawi wa vijana na jamii kwa ujumla”