Wanawake kunufaika kiuchumi kupitia mradi wa TELS

DAR ES SALAAM: Wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wameendelea kunufaika na programu za uwezeshaji zinazolenga kuwajengea uwezo wa kiuchumi kupitia mafunzo ya ujasiriamali na matumizi ya teknolojia za kifedha.
Meneja wa Vodacom Tanzania Foundation, Sandra Oswald, amesema taasisi hiyo inaendelea kutekeleza programu mbalimbali za kuwawezesha wananchi, ikiwemo mradi wa TELS (Thinking Equal, Leading Smart) unaolenga kuwasaidia wafanyabiashara wadogo kuendesha na kukuza biashara zao.
Akizungumza wakati wa Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) katika banda la Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC), Sandra alisema mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Vodacom Tanzania Foundation, CEO Roundtable na TWCC.
Amesema kupitia mradi huo, zaidi ya washiriki 800 tayari wamepatiwa mafunzo yanayohusu uongozi wa biashara, usimamizi wa shughuli za kibiashara, matumizi ya huduma za fedha kidijitali kama M-Pesa na M-Koba pamoja na namna ya kupata fursa za kifedha na mitaji.
“Lengo letu ni kuhakikisha wanawake, vijana na makundi mengine yanafikiwa na kuwezeshwa ili waweze kujenga biashara endelevu na kushiriki kikamilifu katika uchumi,” amesema Sandra.

Ameeleza kuwa kwa ujumla Vodacom Tanzania Foundation imefanikiwa kuwafikia zaidi ya wanawake 500,000 kupitia programu mbalimbali za uwezeshaji wa kiuchumi, huku ikiendelea kushirikiana na wadau kuboresha mazingira yanayosaidia ukuaji wa biashara ndogo na za kati.
Aidha, amesema katika awamu ya kwanza ya mafunzo yaliyofanyika jijini Dodoma, washiriki walipata ujuzi kuhusu misingi ya ujasiriamali, usimamizi wa biashara na matumizi ya huduma za kifedha za kidijitali, hatua ambayo itawasaidia kuongeza ufanisi katika biashara zao.
Katika kuhitimisha shughuli hiyo, Sandra Oswald alitoa vocha mbili zenye thamani ya Sh500,000 kila moja kwa washindi wa mashindano ya TELS Biashara Kiosk, Fatma Omar Kibwana na Fadhila Athumani Mgumia, ili kuwawezesha kuzitumia kama mitaji ya kukuza biashara zao.



