Wanawake Mtwara kupewa mafunzo ya uongozi

ZAIDI ya Wanawake 100 katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara wanatarajiwa kupata mafunzo kuhusu kushiriki kwenye nafasi mbalimbali za uongozi.

Hatua hiyo ni katika kuelekea uchaguzi mdogo wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Oktoba, 2024 na uchaguzi mkuu mwaka 2025.

Hayo yameelezwa leo Septemba 3, wakati wa uzinduzi wa mradi wa Mwanamke Sasa, unaotekelezwa na shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na masuala mbalimbali ya kijamii mkoani Mtwara la FB-Empowerment uliyofanyika kwenye halmashauri hiyo.

Mratibu wa mradi huo, Shakila Hamisi amesema lengo la mradi ni kuongeza idadi ya wanawake kwenye kuwania nafasi hizo lakini kutokana na idadi ndogo ya viongozi iliyopo kwenye halmashauri hiyo hivyo wameona ni vyema kutoa elimu kwa kundi hilo.

SOMA: Wanawake wanauogopa uongozi

Mradi huo ni wa miezi sita kuanzia Agosti 2024 hadi Januari 2025 unaotekelezwa kwa hatua za awali katika kata tatu kwenye halmashauri hiyo ikiwemo Nanguruwe, Kitere na Msangamkuu ambapo kila kata itachukuwa wanawake 40.

“Mtwara Vjijini ina vijiji 110 lakini wenyeviti wa vijiji wanawake ni wawili tu hivyo tumeona ipo haja ya kuwajengea mwanamke na mabinti kuanzia miaka 18 wenye uwezo wa kuzungumza, uthubutu na ujasiri ili tuweze kuongeza hata idadi ya wanawake 50 kati ya wawili waliopo sasa,” amesema Shakila

Diwani wa Kata ya Ndumbwe kwenye halmashauri hiyo, Mahupa Abdul amelitaka shirika hilo kuhakikisha wanawatoa wanawake kwenye imani potofu kwa kudhani kuwa kila anaegombea au kila kongozi lazima awe mshirikina kitu ambacho siyo kweli kwani ushirikina ni jambo ambalo lina athiri na kudumaza jamii.

Akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Mkuu wa Divisheni ya Uwekezaji Viwanda na Biashara wa Halmashauri hiyo, Alfred Mtawali ametoa rai kwa viongozi kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu kwenye mradi huo ili kuleta matokeo yenye tija na kuwa chanzo cha mafanikio.

“Ningependa kutoa angalizo kwa wananchi wetu huu mradi unakuja kwetu ni wa kwetu ningependa sisi viongozi mmealikwa hapa hususani kina mama kuhamasisha wananchi wetu kushiriki kikamilifu ili angalau basi wawe chanzo cha mafanikio,” amesema

Akizungumza kwa niaba ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Ofisa Tarafa wa Tarafa ya Ziwani kwenye halmashauri hiyo, Winfrida Linyembe ameitaka taasisi hiyo kuwa wanapotoa elimu hiyo ni vema wakashirikisha wanawake na wanaume kwa ujla ili wakawe mabalozi wazuri katika kuisemea taasisi.

Habari Zifananazo

Back to top button