Wanawake wahitajika sekta ya anga

DAR ES SALAAM: JUHUDI zaidi zinahitajika kuhakikisha kuna uwiano sawa katika ushiriki wa wanawake na wanaume katika sekta ya anga nchini tofauti na ilivyo sasa, kwani ushiriki wa wanawake ni asilimia 35.08 wakati wanaume ni asilimia 64.92.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Riziki Pembe Juma, akiwa mgeni rasmi kwenye Kongamano la kwanza la Viongozi Wanawake katika Sekta ya Anga (T-WIA) kujadili changamoto na fursa za wanawake kwenye usafiri wa anga, ndani ya Ukumbi wa Hyatt The Kilimanjaro Hotel, jijini Dar es Salaam.

“Usawa wa kijinsia bado haujazingatiwa vyema katika sekta ya anga. Nini kifanyike? Ni lazima mabadiliko yaanze na sisi kisha tuwainue wengine kisekta ikiwemo katika utendaji na utawala,” amesema kiongozi huyo.

Advertisement

Awali, kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Anga Tanzania (TCAA), Hajat Mtumwa Khatib Ameir, amesema T-WIA inatekeleza Falsafa ya Rais Samia Suluhu Hassan ya R4 kwa namna ya kipekee.

“Jukwaa la Wanawake linafaya upatanishi na uelewa yani ‘Reconciliation’. R ya pili ni kujenga mitazamo ya kuwa masuala ya sekta ya anga ni yetu sote yani ‘Rebuild. Tatu ni kuleta mageuzi yani ‘Reform na ya mwisho ni kuwa na ustahimilivu ‘Resilience’,” au amesema makamu huyo.

SOMA: Wajivunia mafanikio usalama wa anga

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Ramadhan Msangi, amesema, kongamano hili haliishii tu katika kusherehekea mafanikio ya wanawake katika sekta ya usafiri wa anga, lakini ni wakati muhimu kwa sekta ya anga katika siku za usoni.

“Leo tunatambua mchango mkubwa wa wanawake katika sekta ya usafiri wa anga. Wanawake waanzilishi ambao walibadilisha mtazamo na kuchukua hatua kuzunguka maeneo ambayo hayajashughulikiwa, ili kuyafanyia kazi na kuwatia moyo wanawake wengine ili kuiga nyayo zao,” amesema Mkuu wa TCAA.

Awali, akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa T-WIA, Maria Memba, amesema, uanzishwaji wa jukwaa hilo umeegemea katika kuwainua wanawake katika utendaji na utawala kwenye sekta ya anga, uliochagizwa na jitihada za kidunia kutaka uwiano sawa katika ushiriki jinsia zote katika sekta ya anga.

“Kwa Bara la Afrika, mnamo Julai 2004 ulipitisha azimio kuu la usawa wa kijinsia barani Afrika, lililolenga kupanua na kukuza kanuni za usawa wa kijinsia kwenye tume ya anga pamoja na taasisi zote kwenye Umoja wa Afrika (AU),

“Mwaka 2016, Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (ACAO), liliunga mkono hoja hiyo ya usawa wa kijinsia katika sekta ya usafiri na anga kupitia Azimio 3930 lililojumuisha ‘Mpango wa Kukuza Usawa wa Kijinsia’ ili kuleta ufanisi zaidi na kuendana na kasi ya ukiaji wa usafiri wa anga,” amesema Maria.

Jukwaa wa T-WIA, limeanzishwa Oktoba 2023, na kukamilisha usajili wake mwaka huu chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani.

SOMA: Mkataba maboresho usafiri wa anga wasainiwa