Wanawake waja na maazimio 5 kuimarisha amani

JUKWAA la Wanawake 2025 limeazimia mambo matano ili kuimarisha amani na mshikamano wa taifa. Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Taifa, Mary Chatanda aliyataja maazimio hayo akihitimisha jukwaa hilo lililofanyika mjini Dodoma.

Chatanda amesema wanawake wataendeleza misingi ya upendo, heshima, mazungumzo ya kuvumiliana na utatuzi wa migogoro, mambo ambayo ndiyo msingi wa amani ya Tanzania. “Kama wazazi na walezi, wanawake tunatambua wajibu wetu wa kuendeleza misingi ya upendo, heshima, mazungumzo ya kuvumiliana na utatuzi wa migogoro. Huu ndio msingi wa amani ya Tanzania,” alisema Chatanda.

Pia, amesema wamejizatiti kuanzisha na kuhimiza majukwaa ya mazungumzo ya amani kwenye familia, mitaa na makundi mbalimbali, ikiwa ni njia pekee ya kuimarisha mshikamano na kuondoa tofauti zinazoleta migawanyiko. “Tumeazimia kuwa mabalozi wa maudhui yanayojenga umoja, kuheshimiana kutunzana na kulinda hadhi ya taifa. Tunapinga taarifa potofu, lugha za chuki na kauli zinazoleta mpasuko katika jamii,” alisema Chatanda.

Ameongeza kuwa, wanatambua umuhimu wa sauti ya wanawake na vijana katika jamii, hivyo wameazimia kuhamasisha, kusaidia na kuinua jamii hasa wanawake ili kuongeza ushiriki wao katika uongozi na majadiliano ya maendeleo katika taifa.

“Pia, tumeazimia kuwa mstari wa mbele kutambua viashiria vya migogoro katika jamii na kutumia hekima, ushawishi na umoja wetu kuhimiza uvumilivu, utulivu, maelewano na mazungumzo yanayojenga. Hatua hizi ndio mwendelezo wa safari yetu ya pamoja ya kujenga jamii yenye amani, utulivu, matumaini na fursa kwa wote,” alifafanua Chatanda.

Vilevile, amesema jukwaa hilo limewakumbusha kuwa mwanamke anapopewa nafasi, amani inashamiri na vijana wanapopewa ujuzi, taifa linang’ara na wanapokuwa na umoja, Tanzania inatabasamu. Ameongeza kuwa, huo ndio msingi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kujenga uchumi shirikishi na kuimarisha amani ya taifa na kujenga taifa lenye fursa kwa wote.

“Katika jukwaa hili tumeona kuwa amani si jambo la kawaida, bali ni kiini cha maendeleo na ustawi wetu. Wachagiza mada wametuhabarisha na kutukumbusha kuwa wanawake ndio msingi wa maadili katika familia na jamii na vijana ndio watendaji wa leo na walinzi wakuu wa amani yetu,” aliongeza. SOMA: UWT:Wapuuzeni wanaopiga kelele,mkapige kura

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button