Wanawake washauriwa kuzingatia vigezo mikopo

DAR ES SALAAM: WATAALAMU na washauri wa masuala ya fedha kutoka Brac Tanzania Limited wamewataka wanawake kuacha kutanguliza shida binafsi wanapohitaji mikopo, badala yake kuzingatia vigezo na masharti ya kisheria.
Wakizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, wataalamu hao wamewataka wanawake kuzingatia elimu ya fedha kabla ya kuchukua mikopo.
Graceana Rimoy, mtaalamu wa mikopo kutoka Shirika la hilo, alisema dhamira yao ni kumfanya mwanamke awe na biashara na uchumi wake uweze kukua.

“Kwasasa tunaona kuna wimbi kubwa la kina mama kuwa na madeni yaliyowazidi, lakini sisi tunahakikisha kabla mwanachama wetu hajapata mkopo amepewa elimu ya fedha,” alisema.
“Akishaelewa namna gani akope, kwa biashara gani na masharti yake, hapo anaweza kufanya maamuzi ya kuchukua mkopo na hivyo kufanya wanachama wetu kuchukua mikopo na uchumi wao kukua,” aliongeza.

Alisema hadi sasa wana jumla ya wanachama zaidi ya 400,00, ambao wanaonyesha matokeo chanya wanapotumia mikopo hiyo.
Kwa upande wake, Sofia Nyanda mtaalamu wa elimu ya fedha kutoka shirika hilo alisema wanashukuru kwani nchini Tanzania wamefanikiwa kwa kiwango kikubwa kutokana na kuwepo kwa shuhuda mbalimbali zinazoelezea namna walivyonufaika.

Alisema kupitia vipengele vilivyopo maarufu kama Livelihood, watu hupewa mitaji na kuchagua aina ya shughuli wanazotaka kufanya kama saluni, ufugaji, kilimo cha mbogamboga na biashara ya chakula.
Aliongeza kuwa wote hao hupewa mafunzo ya namna ya kuendesha biashara zao ili ziweze kuwaletea faida.
“Kupitia hili najivunia kuwa mwanamke kwa sababu ndoto yangu kubwa ni kuhakikisha kila msichana ambaye amekatisha masomo, hasa kwenye mikoa ile ambayo tunafanya kazi, wanarejea madarasani na kutimiza ndoto zao,” alisema Sofia.

Baadhi ya wananchi walionufaika na uwezeshwaji huo wameelezea namna elimu ya fedha ilivyowasaidia kabla ya kupewa mikopo.
Siwema Chuma, mnufaika wa mikopo hiyo, alisema aliwezeshwa kupata mtaji wa biashara ya mama lishe, jambo lililomsaidia kununua vifaa vya kufanyia biashara akiwa na mfanyakazi mmoja, na baadaye biashara hiyo ikaendelea kukua. Kupitia biashara hiyo pia aliweza kuanzisha biashara nyingine.
Naye mnufaika mwingine, Nasra Shafii aliishukuru Brac kwa kumuwezesha kupata mkopo uliomsaidia kufungua migahawa miwili ya mama lishe pamoja na duka la nguo.



