Wanne mbaroni kwa nyara za serikali

JESHI la Polisi mkoani Kagera linawashikilia watu wanne waliojihusisha na ujangili wa nyara za serikali katika Hifadhi ya Taifa ya Ibanda Kyerwa na Rumanyika Karagwe.

Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, William Mwampaghale aliwataja watuhumiwa waliokamatwa na nyara hizo kuwa ni Raphael Lugaira (44), Fikiri Lugaira  (43), Majaliwa Charles (42) na Warwa Rupily (45), wote wakazi wa Wilaya ya Biharamulo.

Alisema uchunguzi ukikamilika watafikishwa mbele ya vyombo vya sheria huku akitoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu unajitokeza na kupoteza mapato ya serikali.

Kwa mujibu wa Kamishina Msaidizi wa Uhifadhi, Hifadhi ya Taifa ya Ibanda Kyerwa, Frederick Mofulu alisema Jeshi la Uhifadhi wa Wanayapori na Misitu kwa kutumia  askari wa hifadhi walipata taarifa za kiintelejensia kuwa kuna wahalifu wanaua wanyama katika hifadhi za taifa ambapo walishirikisha Jeshi la Polisi na kuwakamata watuhumiwa hao.

Alizitaja nyara zilizokamatwa ni meno mawili ya tembo, ngozi ya fisi, kichwa cha fisi, vipande vitatu vya ngozi ya nyati, mkia wa nyati na ngozi ya swala.

Aidha watuhumiwa hao walikamatwa na silaha mbili aina ya gobore pamoja na risasi tatu za kienyeji aina ya gololi ambazo hutumika kuua wanyamapori.

Watuhumiwa wote walikamatwa Februari 13 mwaka huu katika Kijiji cha Muungano, Kata Lusahunga Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera.

Habari Zifananazo

Back to top button