Waomba msaada wamalizie ujenzi wa madarasa

KIGOMA; SHULE ya Msingi Kigadye iliyopo Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma,  inakabiliwa na changamoto kubwa ya mrundikano mkubwa wa wanafunzi darasani, hivyo imeomba serikali na wadau kumalizia ujenzi wa madarasa matano yaliyofikia usawa wa renta ili kupunguza mrundikano huo.

Mwalim Mkuu wa shule hiyo, Amiri Mohamed akizungumza na waandishi wa habari shuleni hapo alisema kuwa kwa sasa shule ina wanafunzi 2500 kati yake wanafunzi 800 wa MEMKWA, huku ikiwa na madarasa nane pekee.

Kutokana na hali hiyo alisema kuwa shule inakabiliwa na changamoto kubwa ya ufundishaji na ujifunzaji, ambapo inabidi sasa wanafunzi wa MEMKWA kusoma kuanzia saa nane mchana hadi saa mbili usiku, ili muda wa kawaida madarasa hayo yaweze kutumiwa na wanafunzi wanaosoma kwenye mfumo rasmi.

Amiri Mohamed Mwalim Mkuu Shule ya Msingi Kigadye wilayani Kasulu

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Heru Shingi, ambaye kijiji cha kigadye ni sehemu ya utawala wake, Juma Bahangaza alisema kuwa kabla ya kufikia kuomba msaada huo walianza jitihada binafsi kwa uongozi wa shule na kijiji kuitisha mikutano na wananchi ambapo madarasa matano yamejengwa yakigharimu  Sh milioni 26.

Akizungumzia changamoto hiyo, Ofisa Elimu Shule ya Msingi na Awali wa Halmashauri ya Wilaya Kasulu, Elestina Chanafi alisema kuwa wanajua changamoto ya shule hiyo na kwa kiasi kikubwa inasababishwa na watu wanaohamishia watoto wao hapo kwa kufuata shughuli za kilimo.

Chanafi  alisema kuwa halmashauri imeiweka shule hiyo kwenye bajeti ya mwaka ujao wa fedha kuweza kumalizia madarasa hayo, lakini pia ipo miradi ya BOOST na miradi mingine ambayo wanaangalia namna ya kuiingizia shule hiyo ili madarasa hayo yaweze kukamilika.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button