WANANCHI wa vijiji vinavyopitiwa na Barabara ya Likuyufusi –Mkenda na nchi jirani ya Msumbiji kwa upande wa Mkoa wa Ruvuma, wameiomba serikali kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami ili kutatua tatizo la usafiri hasa kipindi cha masika.
Wametoa ombi hilo kwa nyakati tofauti mbele ya waandishi wa habari walioko kwenye ziara ya kutembelea miradi ya barabara inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) katika Mkoa wa Ruvuma.
Mkazi wa Kijiji cha Nakawale wilayani Songea, Shaban Kilomoni alisema katika wilaya hiyo kuna fursa nyingi ikiwamo makaa ya mawe, lakini hayajaanza kuchimbwa wala kunufaisha serikali kutokana na tatizo kubwa la miundombinu ya barabara.
“Kukosekana kwa barabara ya lami ni chanzo cha kusuasua kwa maendeleo kwenye maeneo yetu, hali hii imechangia hata usafiri kwenda Songea mjini kuwa mgumu siyo wakati wa masika tu bali hata muda wa kiangazi, madereva wanatumia nafasi hiyo kupandisha nauli kutoka shilingi 3,000 hadi 7,000,” alisema.
Kandedus Mbawala, dereva wa basi linalofanya safari zake kati ya Songea mjini na Mkenda darajani, alieleza kuwa wakati wa masika wanalazimika kutumia kati ya saa tatu hadi nne kufika Songea mjini na kama ingejengwa kwa lami muda huo ungepungua hadi saa moja.
Mrakibu wa Uhamiaji wa kituo cha Mkenda, Upendo Kikudo, alisema watumishi wa serikali ni sehemu ya waathirika wakubwa wa ubovu wa barabara hiyo kwani wanapohitaji kwenda makao makuu ya wilaya na mkoa kikazi, wanalazimika kutumia muda mrefu, hivyo kuathiri shughuli za kuwahudumia wananchi.
Alisema kwa sasa wafanyabiashara wengi wa Msumbiji wanalazimika kutumia Bandari ya Dar es Salaam na kupita mpaka wa Tunduma mkoani Songwe unaounganisha Zambia na Tanzania, badala ya Bandari ya Mtwara na mpaka wa Mkenda na kwenda moja kwa moja nchini Msumbiji, hivyo kuwaongezea gharama kubwa.
Kwa upande wake Meneja wa Tanroads Mkoa wa Ruvuma, Ephatar Mlavi alisema serikali iko mbioni kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami na hadi sasa kazi iliyofanyika ni upembuzi yakinifu.
Alisema serikali kwa kutambua umuhimu wa eneo hilo kiuchumi, katika awamu ya kwanza itaanza kujenga kilometa 60 kutoka Likuyufusi hadi Muhukuru na baadaye itaendelea kujenga kilometa 64 hadi Daraja la Mkenda linalounganisha nchi ya Tanzania na Msumbiji.