Wapandishwa kizimbani kwa kumpiga Mtu risasi

DAR ES SALAAM: WAFANYABIASHARA wawili wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni, Kinondoni, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka matatu ikiwemo kumpiga risasi Gerdat Mfyoa pamoja na kufanya shambulio la mwili.

Washitakiwa hao ni Nahir Nassor na Mundhir Nassor wote wakazi wa Dar es Salaam na walisomewa mashitaka yao na Wakili wa Serikali, Saada Mohamed mbele ya Hakimu Mkazi, Franco Kiswaga.

Mohamed alidai kuwa katika shitaka la kwanza inadaiwa Februari 18, 2023 eneo la Msasani Mtaa wa Uganda ndani ya Wilaya Kinondoni mkoani Dar es Salaam, mshitakiwa Nahir alimpiga risasi Gerdat Mfyoa kwa kutumia bastola aina ya Barrera kwenye bega la kushoto na kumsababishia madhara makubwa.

Katika shitaka la pili alidai kuwa tarehe hiyo na eneo hilo washtakiwa wote walifanya shambulio la mwili kwa kumpiga Salehe Mfyoa, sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia apate majeraha mwilini mwake.

Katika shitaka la tatu alidai kuwa tarehe hiyo na eneo hilo washitakiwa wote walifanya shambulio la mwili kwa kumpiga Neema Mfyoa sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia kupata majeraha mwilini mwake. Washitakiwa wote walikana mashitaka yanayowakabili.

Mohamed alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika hivyo aliiomba Mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea washitakiwa hoja za awali.

Washitakiwa wote waliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na mdhamini mmoja kwa kila mshitakiwa atakayesaini bondi ya sh Milioni tatu.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Oktoba 23, Mwaka huu kwa ajili ya kuwasomea washitakiwa hoja za awali.

Habari Zifananazo

Back to top button