Toshiaki, Mkomwa kortini Dar wizi wa kuaminika

Wapandishwa kortini kwa wizi wa kuaminika

RAIA wa Japan, Toshiaki Aizawa (42) na Hamis  Mkomwa (40), mkazi wa Goba, Dar es Salaam, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka tisa ya wizi wa kuaminika.

Washitakiwa hao wamesomewa mashitaka leo na Wakili wa Serikali, Tumaini Mafuru mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Rhoda Ngimilanga.

Akiwasomea hati ya mashitaka, Mafuru alidai kuwa katika  tarehe isiyofahamika kati ya Septemba, mwaka  2019 hadi Oktoba , mwaka 2020  Aizawa na Mkomwa wakiwa wakurugenzi wa kampuni ya Japan Tanzani Tours katika eneo la Maktaba Ilala, waliiba vifaa  vya ofisi vyenye thamani ya Sh 38,800,00 mali ya kampuni ya Japan Tanzania Tours Limited .

Advertisement

Katika shitaka la pili hadi la sita inadaiwa mshitakiwa, Mkomwa akiwa katika ofisi za mamlaka ya mapato Tanzania zilizopo Kinondoni na Ilala, alibadili umiliki wa magari kutoka kampuni ya Japan Tanzania Tours Limited kwenda katika kampuni yake ya Ada Car Hire Limited na wamiliki wengine.

Inadaiwa Februari 28, mwaka 2019 alibadili usajili wa gari aina ya Toyota  Landcruser lenye namba ya usajili T 654 BJX yenye thamani ya Sh 30,801,460 kwenda kwa Ada Car Hire Limited na Aprili 10, mwaka 2019 alibadili usajili wa gari aina ya Toyota Rav4 yenye namba ya usajili T 178 BBB yenye thamani ya Sh  28,543,328 kwenda kwa Edger Maganga.

Pia kati ya Machi 14,  mwaka 2019 na Aprili 11, mwaka 2019 Mkomwa alibadili umiliki wa magari aina ya Nissan Pickup yenye namba ya usajili T 738 DJU yenye thamani ya Sh 57,289,353 kwenda kwa Tatsuo Fumio Hasegawa, Toyota Rav4 yenye namba ya usajili T 205 BZS yenye thamani ya Sh 15,000,000 kwenda kwa Invocavity Timoth Nkya na Toyota Harrier yenye namba ya usajili T 325 AYC yenye thamani ya Sh 14,527,279 kwenda kwa kampuni ya Genk Car Rental.

Katika shitaka la saba hadi la tisa inadaiwa kuwa Septemba 3, mwaka 2019 na Novemba 5, mwaka 2019  katika benki ya Stanbic iliyopo Wilaya ya Ilala aliiba kwa kujihamishia fedha kiasi cha dola 17,085.6 kutoka katika akaunti ya Japan Tanzania Tours Limited kwenda kwenye akaunti ya kampuni Ada Car Hire Limited  iliyopo katika benki ya  CRDB.

Mafuru alidai kuwa upelelezi aujakamilika na kuiomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Washitakiwa wote walikana mashitaka yao na kurudishwa rumande hadi Januari 10, mwaka 2023 baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili pamoja na Mkomwa kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya shilingi 218,000,000 au fedha tasilimu Sh 109,000,000 na Aizawa kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh 16,000, 000 au fedha tasilimu 16,000,000

1 comments

Comments are closed.