Wapendekeza mikutano ya hadhara iruhusiwe

Uwepo mjadala kitaifa kabla ya Katiba mpya

KIKOSI Kazi cha kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi kilichoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kimetoa mapendekezo mbalimbali ikiwamo yanayotaka mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa nchini iruhusiwe kufanyika.

Hayo yalibainishwa na Mwenyekiti wa Kikosi Kazi hicho, Profesa Rwekaza Mukandala, wakati akikabidhi ripoti yao kwa Rais Samia jana Ikulu, Dar es Salaam.

Profesa Mukandala alisema kikosi kazi kilipendekeza mikutano hiyo ya hadhara iruhusiwe kufanyika kwa mujibu wa katiba na sheria.

Advertisement

Pia alisema kilipendekeza mikutano ya ndani ya vyama vya siasa pia iendelee kufanyika bila vikwazo vyovyote.

“Yafanyike marekebisho ya sheria ili kuhakikisha mikutano ya hadhara inafanyika kwa ufanisi, sheria hizo ni pamoja na Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258, Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma Saidizi Sura 322, Kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa za mwaka 2019,” alisema Profesa Mukandala.

Kuhusu demokrasia ndani ya vyama vya siasa, kikosi kilipendekeza sheria ya vyama vya siasa ifanyiwe marekebisho ili kulipatia Baraza la Vyama vya Siasa linaloundwa na vyama vyenyewe, mamlaka ya kushughulikia suala la uvunjifu wa maadili ya vyama kupitia kamati yake ya maadili.

Profesa Mukandala alitaja mapendekezo mengine ni pamoja na Msajili wa Vyama vya Siasa kuandaa mwongozo wa uchaguzi wa ndani wa vyama vya siasa, kuweka masharti kwamba idadi ya jinsi moja katika vyombo vya uamuzi vya chama cha siasa isipungue asilimia 40.

Yametaka pia chama cha siasa kuwa na sera ya ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika shughuli zake.

Kuhusu ruzuku inayotolewa na serikali kwa vyama vya siasa, kikosi kazi kimependekeza kuwa mfumo wa sasa wa kugawa ruzuku ya serikali kwa vyama vya siasa uendelee isipokuwa asilimia 10 ya fedha za ruzuku kwa vyama vya siasa inayotengwa katika bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha husika igawiwe sawa kwa vyama vyote vya siasa vyenye usajili kamili kwa mujibu wa vigezo na masharti.

Profesa Mukandala alitaja vigezo na masharti hayo kuwa ni pamoja na chama kuwa na usajili kamili, chama kiwe kimefanyiwa uhakiki na msajili wa vyama vya siasa na kukidhi vigezo vya usajili kamili.

Vilevile chama kiwe kimeshiriki uchaguzi mkuu walau mara mbili tangu kipate usajili kamili, kisiwe kimepata hati chafu katika mwaka wa fedha uliopita na ruzuku itumike kwa ajili ya kuendesha ofisi ya makao makuu, ofisi ndogo au ofisi kuu ya makao makuu ya chama husika.

Kikosi kazi kimependekeza pia sheria ya vyama vya siasa itamke kuwa asilimia 20 ya fedha za ruzuku ya serikali kwa vyama vya siasa kwa mwaka wa fedha igawiwe kwa vyama vya siasa vyenye madiwani wa kuchaguliwa katika kata kwa uwiano wa madiwani badala ya kumwachia waziri mwenye dhamana kuamua.