Wapewa mafunzo kupima usikivu kwa watoto

Wapewa mafunzo kupima usikivu kwa watoto

HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili, imeanza kutoa mafunzo kwa wauguzi katika Hospitali ya Rufaa ya Bombo iliyoko mkoani Tanga ya kubaini tatizo la usikivu kwa watoto wachanga, ili kuwapatia matibabu wakiwa hatua za awali.

Akizungumza na waandishi wa habari, daktari bingwa wa magonjwa ya masikio, pua na koo kutoka  Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,  Dk  Edwin Liyombo, amesema kuwa takwimu walizozifanya zinaonesha kati ya watoto 100 wanaozaliwa, saba wamebainika kuzaliwa na tatizo la usikivu.

Amesema kuwa mafunzo hayo yataweza kusaidia kubaini tatizo la usikivu kwa mtoto likiwa katika hatua za awali, hivyo kupatiwa matibabu na kuweza kurudi katika hali nzuri.

Advertisement

“Tumekuwa tukiwawekea watoto vifaa vya usaidizi wa kusikia, lakini iwapo kama wangeweza kubaini changamoto hiyo mapema ingeweza kutibika,ndio maana tumeona tushuke huku katika hospitali za mikoa, ili kueneza utaalamu huo,”amesema Dk Liyombo.

Amesema kwamba wameamua kuwafundisha wauguzi programu ya kupima usikivu kwa watoto wanaozaliwa, ili kuweza kuwasaidia watoto wanaokuwa na shida hiyo pindi wanapozaliwa.

Amesema kwa sababu kuna mashine maalumu ya kuwapima kama wana matatizo na wakibainika mapema inawasaidia kuweza kuona namna ya kulipatia ufumbuzi.

“Tunawafundisha wauguzi jinsi ya kufanya uchunguzi na baadae itakwenda nchi nzima, kwani hawa tunaowafundisha baadae watakuwa walimu na kufundisha wengine, lakini tutawaleta mashine ndogo itakayotumika kupima watoto wanapozaliwa,” amesema Dk Liyombo.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *