MSUMBIJI : WAPINZANI wa Msumbiji wamejipanga kwa maandamano makubwa kabla ya kutangazwa kwa matokeo ya mwisho ya uchaguzi mkuu, ambayo yanaonekana kuwa na utata mkubwa.
Matokeo hayo yanatarajiwa kutangazwa Jumatatu ijayo, lakini kiongozi wa upinzani, Venancio Mondlane, ameweka wazi kwamba ataitisha maandamano na vurugu nchini kote ikiwa Baraza la Kikatiba litaidhinisha matokeo ya awali yaliyomuweka katika nafasi ya pili kwenye uchaguzi wa Oktoba 9.
Tangu matokeo ya awali kutangazwa, nchi hiyo imekuwa katika machafuko makubwa ambayo yamesababisha vifo vya watu 130 na uharibifu mkubwa wa miundombinu muhimu.
Ghasia hizo zimevuruga shughuli za kibiashara mijini, na kuathiri uzalishaji wa viwandani, hali ambayo imezidi kuzorotesha uchumi wa nchi. SOMA: Jeshi,Polisi wadhibiti maandamano Msumbiji
Hali hiyo imesababisha Serikali ya Marekani kutoa tahadhari kwa raia wake, ikiwasihi kuahirisha safari zao kuelekea Msumbiji kwa sasa, kwa kigezo cha nchi kuingia katika machafuko makubwa ya kisiasa.
Katika hali hii, masuala ya usalama na utulivu wa kijamii yanaonekana kuwa tishio kuu kwa ustawi wa nchi.