DAR ES SALAAM – WAZIRI Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Warioba amezitaka mamlaka za serikali na vyama vya siasa kujadili kwa njia ya amani ili kuondoa mivutano ya kisiasa kabla ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliopangwa kufanyika mwezi Novemba.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Jaji Warioba amesisitiza kuwa majadiliano ni muhimu katika kutatua migogoro ya kisiasa na kwamba taifa linahitaji masikilizano ili kujenga msingi thabiti wa maendeleo.
“Taifa linahitaji masikilizano, ndio msingi mkubwa wa kujenga taifa … kufanya majadiliano mezani ndio dira ya kulikomboa taifa na hakuna sababu ya mivutano kwa sababu haina tija kwa maendeleo ya taifa,” amesema Warioba.
Aidha, alikumbusha kuhusu changamoto zilizojitokeza katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2019/2020, ambapo alisema usimamizi wa uchaguzi haukuenda vizuri na kulikuwa na tuhuma za rushwa miongoni mwa wagombea na wasimamizi.
“Uhamasishaji ulikuwa mkubwa lakini wananchi waligoma kwenda kupiga kura, ishara ya kutokuwa na imani na uchaguzi,” alisisitizaWarioba.
Warioba pia alikosoa tabia ya wagombea kutumia rushwa ili kupata nafasi za uchaguzi, akisema,
“Kuna haja kwa vyama vya siasa kuchagua wawakilishi bora ambao watashughulikia maslahi ya taifa na sio maslahi binafsi.”
Katika wito wake kwa wananchi, Warioba aliwasihi kuendelea kujifunza kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kujitokeza kwa wingi kupiga kura ili kuchagua viongozi watakaoweza kuleta maendeleo katika jamii zao.
“Zimebaki siku chache, Tume ya Uchaguzi kwa kushirikiana na Ofisi za Tamisemi inapaswa kuendelea kuwaelimisha watanzania kuhusu umuhimu wa kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura na faida za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa,” aliongeza.
SOMA: Takukuru kutoa elimu ya rushwa uchaguzi mitaa
Jaji Mstaafu Warioba alihitimisha akisisitiza kwamba ni muhimu kwa wananchi kufanya maamuzi sahihi bila ushawishi wowote ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa haki na wa amani.