Wasambazaji mbolea wasio waadilifu wasakwe

TAKWIMU zinaonesha Tanzania imepiga hatua kubwa katika uzalishaji wa chakula nchini kiasi kwamba sasa taifa linajitosheleza kwa chakula kwa ziada ya zaidi ya asilimia 120 inayohusu mazao makuu nchini kama mahindi, mchele, mtama, uwele, ulezi, ngano, ndizi, muhogo, viazi vitamu, viazi mviringo, maharage na mikunde.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa uzalishaji wa chakula kwa msimu wa kilimo wa 2022/2023 ulitosheleza mahitaji ya chakula ya tani 16,390,404 kwa mwaka 2023/2024 na kuwepo kwa ziada ya tani 4,011,611.

Kutokana na hali hiyo, taifa limejitosheleza kwa chakula kwa asilimia 124 ikilinganishwa na utoshelevu wa asilimia
114 mwaka 2022/2023. Aidha, utoshelevu wa chakula unatarajiwa kufikia asilimia 130 ifikapo mwaka 2025.

Advertisement

Kuna sababu nyingi zilizowezesha mafanikio haya makubwa ikiwemo sera nzuri na mikakati ya serikali chini ya Wizara ya Kilimo katika kuhakikisha kilimo ambacho kinategemewa na Watanzania wengi, kinaleta tija kwao na kwa taifa kwa ujumla.

Miongoni mwa mambo hayo ni matumizi ya mbegu bora, kuimarishwa kwa mifumo ya kilimo cha umwagiliaji,
matumizi ya mbolea ya ruzuku na kuwapo kwa wataalamu wa kutosha katika maeneo mbalimbali nchini.

Hata hivyo, kumekuwapo na changamoto katika baadhi ya masuala ya usimamizi ikiwamo mifumo ya usambazaji wa mbolea kiasi cha Bunge kuiagiza serikali kupitia Wizara ya Kilimo na Mamlaka ya Udhibiti Mbolea Tanzania (TFRA) ziimarishe mifumo ya usambazaji wa mbolea.

Kwa mujibu wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), mifumo hiyo iimarishwe kwa kuzingatia ubora, bei elekezi na kuwafikia wakulima kwa wakati.

Kamati hiyo imeagiza hatua stahiki zichukuliwe kwa wasambazaji wa mbolea ambao watagundulika kuwa wanauza mbolea bila kuzingatia miongozo ya usambazaji wa mbolea kwa wakulima nchini inayokuwa imetolewa na serikali.

Tunaunga mkono maagizo haya ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya PAC kutokana na ukweli kuwa serikali imetoa
fedha nyingi katika ruzuku ya mbolea ili kuhakikisha wakulima wananufaika na hatua hii yenye lengo la kuongeza uzalishaji na tija.

Kwa hiyo, endapo usimamizi hautakuwa nzuri utasababisha wakulima kuuziwa mbolea zisizo na viwango na ubora, na hivyo kusababisha uzalishaji kupungua au kushuka kwa kiwango kikubwa, jambo ambalo halikubaliki.

Kuruhusu wasambazaji hawa wa mbolea kuuza mbolea visizo na viwango na nyingine ambazo hazijasajiliwa ni
uhujumu wa uchumi, hivyo TFRA inapaswa kuwa macho na kuhakikisha wahusika wanachukuliwa hatua kali ikiwamo kuwafutia leseni zao.

Tunaamini Wizara ya Kilimo na TFRA watazifanyia kazi changamoto zote zilizotajwa na Kamati ya Bunge ili wakulima wasiendelee kuhujumiwa, kwani chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ameweka mkazo katika kilimo, amewekeza fedha nyingi katika sekta hii.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *