Washerehekea Idd na milio ya risasi

WAKAZI wa Khartoum nchini Sudan wamesherehekea Sikukuu ya Idd huku milio ya risasi ikisikika pamoja na kuwa wapiganaji wa pande mbili walitangaza kusitisha mapigano.

Hofu iliyotanda kwa wakazi wa mji huo ilifanya washindwe hata kutoka kwenda kusherehekea sikukuu hiyo kama ambavyo wamezoea kufanya nyakati nyingine.

“Ni kama siyo Idd, barabara ni tupu, watu wana hofu na usiku wa jana hatukulala kwa sababu ya milio ya risasi iliyokuwa ikisika,” alisema mmoja wa wakazi wa mji huo, Zahra Saeed.

Wengine walisema walishindwa hata kuhudhuria sala ya pamoja ambayo ndiyo sehemu muhimu ya siku hiyo kutokana na hofu ya kukutwa na mashambulizi ya wapiganaji hao.

“Kwa mara ya kwanza nimeshindwa kuhudhuria, badala yake watu wengine wamesali majumbani mwao, sasa hivi mapigano yanaendelea, hawaheshimu watu, hawaheshimu umuhimu wa tukio hilo,” alisema Walaa Ibrahimu ambaye alikuwa ni mwanafunzi wa udaktari.

Sudan imekuwa katika machafuko kwa wiki 10 mfululizo yaliyoanza Aprili mwaka huu kati ya Majeshi ya Serikali ya Sudan na kundi ya wapiganaji la Rapid Support Forces (RSF).

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa zaidi ya watu 500,000 wamekimbia Sudan katika kipindi cha wiki moja iliyopita huku ikikadiriwa kuwa watu zaidi ya milioni 2 wamekimbia makazi yao nchini humo.

Inaelezwa kuwa kumekuwa na uvamizi majumbani na kwenye maeneo ya biashara katika kipindi hicho cha machafuko yakiambatana na unyang’anyi wa kutumia silaha.

Habari Zifananazo

Back to top button