Washindwa kuchota maji ya bomba kwa kukosa muuzaji

KATAVI: Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Katavi, Idd Kimanta ametoa siku mbili kupatikana huduma ya maji katika Kijiji cha Wachawaseme kilichopo Kata ya Utende Halmashauri ya Mlele kutokana na kukosekana kwa msimamizi wa gati la maji na kulazimika kutafuta maji visimani kwa umbali mrefu.

Maagizo hayo yametokana na malalamiko kutoka kwa wanakijiji cha Wachawaseme,wakati Mwenyekiti Kimata alipofanya mkutano wa hadhara kijijini hapo, ambapo walimweleza changamoto ya kufungiwa maji kutokana na kukosekana msimamizi na muuzaji wa maji kwa zaidi ya miezi sita.

“Watu wanahangaika na maji yamefungwa kwa sababu eti hakuna wa kusimamia kuuza,Mkuu wa Wilaya (Majid Mwanga) nataka kesho kutwa Chama Cha Mapinduzi kijue maji hapa yamefunguliwa,mtu wa RUWASA kama umekosa mtu wa kusimamia watu watachota bure” amesema Kimanta

Nae kaimu Meneja wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira (RUWASA) Wilaya ya Mlele, Madaha Majagi, amekiri kutokuwepo kwa mtoa huduma na kufungwa kwa bomba la maji kutokana na makubaliano waliyoyafanya kati ya wananchi na chombo cha watoa huduma ya maji ngazi ya jamii (CBWSOs).

“Hatuwezi kuyasimamia maji yatoke bila msimamizi,na msimamizi anapatikana kwa mfumo wao weyewe kama jamii” amesema Majagi.

Awali wananchi hao walisema kuwa kutokana na kukosekana muuzaji na kupelekea kufungiwa maji hulazimika kutafuta maji ya kutumia kisimani ambapo maji hayo si salama kwa afya zao.

Habari Zifananazo

Back to top button