Washukuru kwa kupatiwa mikopo Mpanda

Washukuru kwa kupatiwa mikopo Mpanda

KIKUNDI cha watu wenye ulemavu kinachojihusisha na ushonaji viatu cha Pcohekago Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi, kimemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwawezesha walemavu kunufaika na mikopo inayotolewa na Halmashauri, ambapo mpaka sasa kimekopeshwa Sh milioni 19 kwa nyakati tofauti.

Salamu za shukurani zimetolewa na kikundi hicho, wakati kilipotembelewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), ikiongozwa na Stanslaus Mabula kwa ajili ya kukagua maendeleo ya kikundi hicho.

Advertisement

Akisoma taarifa Mwenyekiti wa kikundi hicho, Plasido Kameme, amesema awali kikundi kilikopa Sh milioni 8 mwaka 2019/2020 na kuzitumia kushona viatu na kubrashi, kushona na kuuza nguo, kununua na kuuza mazao, ambapo kikundi kilifanikiwa kurejesha fedha kwa wakati.

Ameeleza mwaka wa fedha wa 2020/2021 kikundi kilipokea mkopo awamu ya pili Sh milioni 11, ambazo zinaendelea kutumika kuendeleza biashara walizonazo.

Amesema faida waliyoipata kutokana na mikopo imewawezesha kujenga nyumba za kuishi kila mwanakikundi na kuboresha miradi yao.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa LAAC, Stanslaus Mabula amepongeza kikundi kwa kutumia fursa ya kujiunga kwenye vikundi kwa kupata mikopo ambayo haina riba. 

Ameridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Manispaa ya Mpanda hasa ya utoaji wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.