Wasioendeleza ardhi Kigamboni kunyang’anywa

MKUU wa Wilaya ya Kigamboni, Halima Bulembo amesema yeyote mwenye ardhi isiyoendelezwa wilayani humo itachukuliwa na serikali kwakuwa ni ukiukwaji wa sheria ya ardhi

Kauli hiyo imetolewa leo Juni 02, 2023 wakati akisikiliza na kutatua kero za wananchi wa mtaa wa Kichangani, Kata ya Pemba Mnazi, wilayani humo katika ziara ya kikazi.

“Niwatake wananchi wa Kigamboni yeyote mwenye ardhi ambayo haijaendelezwa wilayani Kigamboni waendeleze, wasipoendeleza tutapitia sheria ya ardhi tukijiridhisha tutachukua maeneo hayo,”  amesema.

Pia katika kuondoa kero ya uhaba wa choo katika shule ya msingi Kichangani,  DC Bulembo amechangia mifuko 20 ya saruji.

“Ninachangia mifuko 20 kutatua changamoto za vyoo, na nikitoa mimi Mkuu wa Wilaya ametoa Rais mama Samia,”  amesema.

Kwa upande mwingine Mkuu huyo wa Wilaya ameahidi kuwachukulia hatua mwananchi yeyote wilayani Kigamboni atakayehusika na uharibifu wa mazingira.

“Yeyote tutakayemkuta anachoma miti na kukata mkaa tutamkamata, na kama alikuwa hajui kuanzia leo Juni 02 namwambia ni kosa na ni marufuku,”  amesema.

Pia amewataka wananchi kuwa chachu ya ulinzi na usalama wao kwa kukomeaha vitendo vya kihalifu ikiwemo wizi.

“Hapa Kichangani kuna wizi, watu hawakai kwa amani, wizi ni kosa. Nikiwa Mweyekiti wa ulinzi na usalama wa wilaya siwezi kumvumilia mtu yeyote atakayejishughulisha na vitendo vya wizi ukibainika tutakukamata,”  amesema.

Huu ni muendelezo wa DC Bulembo kutatua changamoto za wananchi kwa kufanya ziara aliyoiita Mtaa kwa Mtaa kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero wilayani humo.

Habari Zifananazo

Back to top button