DODOMA; NI Stephen Wasira. Pengine hivyo ndivyo unavyoweza kujibu lile swali la nani atakuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, swali lililokuwa likiulizwa na makada wa CCM na hata wafuatiliaji wa karibu wa siasa nchini, hasa mwaka huu ambao Tanzania itafanya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani .
Mengi yamesemwa na wengi wametajwa wakihusishwa na nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara iliyokuwa ikishikiliwa na komredi Abdulrahman Kinana, ambaye ameamua kupumzika.

Mchakato wa kujaza nafasi iliyoachwa na Kinana, unafanyika baada ya kikao cha Kamati Kuu ya CCM jana Januari 17 na kutoka na mapendekezo yaliyowasilishwa kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM iliyokutana pia jana, ambayo nayo imewasilisha jina hilo kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu kwa ajili ya kupigiwa kura ya ndio au hapana.
Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan ametamka jina hilo kwenye Mkutano Mkuu wa CCM leo mkoani Dodoma, ambapo wajumbe watapiga kura ya ndiyo au hapana.
Wasira amewahi kushika nyadhifa mbalimbali baada ya kuingia kwa mara ya kwanza bungeni mwaka 1970 jimbo la Mwibara akiwa na umri wa miaka 25 na aliteuliwa na Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere kuwa Naibu Waziri wa Kilimo.

Mwaka 1985 alichaguliwa kuwa Mbunge wa Bunda, baada ya jimbo hilo kugawanywa na Mwibara, ambapo Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi alimteua kuwa Naibu wa Waziri wa Serikali za Mitaa na baadaye Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo.
Mwaka 1995 Wasira aliwania ubunge wa Bunda kupitia CCM, lakini alishindwa kwenye kura za maoni na Joseph Warioba, Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais Mstaafu, hivyo Wassira akaondoka CCM na kuhamia Chama cha NCCR Mageuzi. Alipeperusha bendera ya chama hicha katika uchaguzi wa ubunge na kumuangusha Warioba.
Hata hivyo CCM kupitia mgombea wake, Jaji Warioba ilipinga matokeo hayo mahakamani ambako Mahakama Kuu Mwanza ilitengua ubunge wa Mzee Wasira. Uchaguzi wa marudio ulifanyika mwaka 1999 na baada ya uchaguzi huo Wasira alijiunga tena na CCM.
Uchaguzi wa mwaka 2005 alijitosa Jimbo la Bunda na alishinda kura za maoni ndani ya CCM na kuwa mgombea katika jimbo hilo ambako katika Uchaguzi Mkuu alipita bila kupingwa, akatangazwa kuwa mbunge.Rais Jakaya Kikwete alimteua kuwa Waziri wa Maji Januari 2006- Oktoba 2006.
Kati ya Novemba 2006 – Novemba 2010 alikuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, lakini Februari–Mei 2008 aliwahi kutumikia kwa muda Ofisi ya Waziri Mkuu akiwa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Uchaguzi wa mwaka 2010, Wasira aligombea tena ubunge wa Bunda na kushinda kwa asilimia 66.1 na Rais Kikwete akamteua kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Uhusiano na Uratibu kabla ya kurudishwa kuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.
Pia amepata kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya chama, ikiwemo Mjumbe wa Kamati Kuu na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC). Alikuwa miongoni mwa wana CCM waliochukua fomu kuomba kuteuliwa kuwania urais mwaka 2015, ambapo Dk John Magufuli aliteuliwa kupeperusha bendera ya CCM.