ZANZIBAR: WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amewaonya wanafunzi dhidi ya kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara baada ya kufungua kikundi cha ujasiriamali visiwani Zanzibar. Kikundi hicho kinajumuisha makundi mbalimbali ikiwamo kundi la vijana ambalo limekuwa likiathirika na matumizi ya dawa za kulevya kwa njia ya kuvuta puani, mdomoni na kujidunga sindano.
“Ni muhimu kwa jamii nzima kushikamana ili kupambana na matumizi ya dawa za kulevya, tafiti zinaonysha sasa janga la matumizi ya dawa za kulevya limehamia kwa wanafunzi ambao wengine wana digrii zao lakini wamejiingiza katika uraibu wa dawa za kulevya,”alisema Masauni.
Aliongeza: “Jambo hili linahatarisha uhai wa taifa kwani vijana ni nguvu kazi ya taifa lolote lile duniani, sisi kwa upande wa serikali tumeunganisha nguvu ya pamoja katika kudhibiti uingiaji wa dawa za kulevya na wito wangu kwa wazazi na wanajamii kuhakikisha wanashirikiana na serikali katika kudhibiti janga hilo”.
Taarifa zinabainisha waraibu wa dawa za kulevya wamekuja na mtindo wa kutumia dawa za kutibu binadamu kama mbadala.
Masauni alizungumzia pia vitendo vya udhalilishaji vinavyoendelea kukithiri huku jamii na familia wakiendelea kuwaficha watu wenye kujihusisha navyo.
Ameiasa jamii itoe taarifa kwa Jeshi la Polisi waonapo dalili za udhalilishaji wa kijinsia kwa watoto na makundi mbalimbali.
‘Kuna mmomonyoko wa maadili unaosababisha matukio ya ukiukwaji wa maadili hayo ikiwamo unyanyasaji wa kijinsia, ubakaji, ulawiti na ushoga; mambo hayo hayajaisha katika jamii yetu na ni muhimu kwa jamii nzima kushikamana ili kupambana na majanga haya,” alisema.
“Kumekuwa na desturi kwa baadhi ya watu wanaofanya matendo ya ubakaji na ulawiti hususani kwa watoto, tunawakumbatia na kuwaficha. Imefikia hatua mtu amethibitika kufanya ulawiti lakini wanamficha katika kuhakikisha yule mtuhumiwa haendi kwenye mikono ya sheria hiyo.
SOMA: Wanachuo watumiaji wakubwa dawa za kulevya