NCHI wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimeombwa kuweka utaratibu maalumu kuwezesha wajasiriamali wadogo kuvuka mipaka ya nchi zao kutafuta fursa kama masoko na rasilimali ndani ya jumuiya.
Mchambuzi wa masuala ya diplomasia na uchumi, Profesa Wetengere Kitojo na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye pia ni Mtaalamu wa Uchumi, Profesa Humphrey Moshi, walisema hayo jana zikiwa zimebaki siku chache kabla ya kufanyika kwa Kongamano la Utalii la EAC nchini Burundi.
Wamesema ili kuondoa vikwazo vinavyowakabili wajasiriamali na kuwafanya wahudhurie makongamano mbalimbali ndani ya EAC, utafiti unatakiwa kufanyika ili kubainisha vikwazo hivyo na kuvifanyia kazi kwa haraka.
Profesa Wetengere alisema ni muhimu kila nchi kutoa mitaji kwa wajasiriamali na kuweka utaratibu imara wa kufuatilia na kuwajulisha wajasiriamali husika namna wanavyoweza kufaidika na fursa zilizopo.
“Serikali ziweke mazingira rafiki ya kulinda mitaji ya wajasiriamali ili waione jumuia kama taasisi ya kulinda na kuboresha biashara zao badala ya kuiona jumuiya kama chombo cha kuua mitaji yao,” alisema Profesa Wetengere.
Profesa Moshi alisema vikwazo vilivyopo kati ya nchi na nchi ndani ya EAC si rafiki kwa wajasiriamali wenye utashi wa kujikwamua kutoka kipato kidogo kwenda cha juu.
Alisema jumuiya hiyo kwa pamoja na nchi washirika inapaswa kuweka utaratibu utakaokuwa rafiki kwa wajasiriamali wenye mitaji midogo ili watafute fursa nje ya mipaka ya nchi zao ndani ya EAC kama ilivyo kwa wafanyabiashara na wawekezaji wenye mitaji mikubwa.
Wakizungumza na HabariLEO Afrika Mashariki kuhusu uzoefu waliopata katika Maonesho ya Biashara ya Bidhaa za Ubunifu na Kilimo ya EAC yaliyofanyika Mwanza Augosti 26 hadi Septemba 4, mwaka huu, baadhi ya washiriki kutoka nchi hizo walisema wanatamani kufanyabiashara ya kuvuka mipaka ya nchi zao katika EAC, lakini wanakwamishwa na udogo wa mitaji yao.
Vikwazo vingine walisema ni hofu ya kupata hasara pamoja na kutokujiamini miongoni mwa wafanyabiashara na wajasiriamali hao wenyewe.
Priscar Lanyero kutoka Uganda anayejishughulisha na utengenezaji wa mikoba, bangili za mkononi, vikapu pamoja na ushonaji wa mabegi alisema:
“Asilimia kubwa ya wajasiriamali wa Afrika Mashariki wanapenda kufanya biashara zinazovuka mipaka kutoka katika mataifa yao ili kujitanua kibiashara na kutafuta masoko, lakini wanashindwa kwa sababu ya mitaji kuwa midogo.”
Kwa mujibu wa Lanyero, anashiriki katika maonesho hayo akitegemea kupata faida kubwa na biashara yake itakuwa kubwa na kupaa kutokana na ushiriki wa mataifa yote ya Afrika Mashariki ambayo ni Tanzania, Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Naye Thadeo Ng’oto anayejishughulisha na biashara ya mazao, alisema kuendelea kuogopa hasara na kutothubutu kujaribu kwa wajasiriamali kutasababisha kuendelea kudumaa kibiashara kwa kuwa biashara zao hazitaweza kukua kutokana na kutopata changamoto mpya sokoni.
Kaulimbiu ya maonesho ya mwaka huu ni ‘Lugha ya Kiswahili nguzo mahususi katika kukuza na kuendeleza biashara, viwanda na kilimo Afrika.
Kongamano hilo linalotarajiwa kufanyika Septemba 23 hadi 26 mwaka, katika Mji Mkuu wa Burundi, Bujumbura likishirikisha wajasiriamali kutoka nchi za EAC.
Na Mwandishi Maalumu
MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amewaasa Watanzania wanaoishi Marekani waendelee kuitangaza Tanzania, wavutie wawekezaji na wao wachangamkie fursa za kuwekeza nchini.
Dk Mpango pia amewataka Watanzania hao wafanye juhudi kutafuta masoko ya bidhaa na malighafi za Tanzania katika nchi wanazoishi kwa manufaa ya Watanzania walio wengi.
Alisema hayo jana katika ukumbi wa ubalozi wa Tanzania jijini New York alipokutana na kuzungumza na jumuiya ya Watanzania wanaoishi jijini humo nchini Marekani.
Dk Mpango yupo nchini humo kumwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Baraza Kuu la 77 la Umoja wa Mataifa (UNGA).
Aliwapongweza Watanzania hao kwa jitihada za kuchangia maendeleo katika sekta mbalimbali na akasema Serikali ya Awamu ya Sita inatambua mchango wa wana diaspora hao na itaendelea kuunga mkono jitihada wanazofanya.
Dk Mpango Diaspora wanapaswa kuendeleza lugha ya Kiswahili kwa kuitangaza na kuanzisha vituo vya kujifunzia lugha hiyo katika maeneo waliopo.
Alisema suala la utangazaji wa lugha ya Kiswahili linapaswa kwenda sambamba na kutangaza utamaduni wa taifa la Tanzania na vivutio vilivyopo.
Dk Mpango amewasihi Watanzania waishio Marekani na duniani kote kwa ujumla kuhakikisha wanaishi kwa kuzingatia sheria katika nchi hizo na kujiepusha na vitendo vya kihalifu vitakavyoharibu taswira ya Tanzania.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula alisema wizara hiyo ipo kwenye mchakato wa kutengeneza sera ya mambo ya nje inayotambua mchango wa diaspora.
Aidha alisema wizara itazindua kanzu data itakayowezesha wanadiaspora kutambulika popote walipo duniani.
Awali Mwanzilishi wa Jumuiya ya Watanzania jijini New York Profesa Estomiah Mtui aliishukuru serikali kwa utaratibu uliowawezesha kupata vitambulisho vya taifa na kuendelea kushughulikia suala la hadhi maalumu kwa diaspora.