wataalamu 132 wahitimu mafunzo

Ni ya kukabiliana na milipuko, majanga

WATAALAMU kutoka sekta mbali mbali wamehitimu mafunzo ya kukabiliana na milipuko ya magonjwa pamoja na majanga.

Kozi hiyo  imeendeshwa na Shirika la Afya |Duniani (WHO) kwa kushirikiana na  Kituo cha Udhibiti wa Magonjwa nchini Tanzania (Centre of Diseases Control – CDC) na Wizara ya Afya.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mwakilishi Mkaazi wa WHO nchini Zabloni Yoti amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwa nchi za Afrika kunatokea majanga 150 kwa mwaka sawa na kila baada ya siku nne janga linatokea ama mlipuko wa Ebola Gunea, ama Kongo au Uganda, Marburg Kagera, mlipuko wa kipindupindu Malawi na majanga mengine mengi.

Amesema,  asilimia 70 ya magonjwa ya milipuko yanayowapata binadamu yanatoka kwa wanyama hivyo usalama wa afya ni kipaumbele cha dunia na kama nchi inahitaji kujengewa uelewa kwa kushirikisha sekta zote.

Amesema ni vyema kuwalinda wananchi na dharura na majanga kwani mabadiliko ya tabia nchi nayo huchangia magonjwa ya milipuko

“WHO tunatoa mafunzo haya lengo ni kusevu maisha ya watu, kila nchi lazima iwe na timu kubwa ya wataalamu, janga linapotokea basi waweze kudhibiti kwa haraka, kama sasa hivi kuna timu imetoka miongoni mwa wahitimu hapa wameenda Kagera kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa Marburg.”Amesema

Amesema kundi hilo la wataalamu 132 linaingizwa kwenye ‘data base’ ya WHO na  inapotokea majanga kwenye nchi yoyote basi wanaitwa kwa wakati mmoja ili kwenda kuokoa.

Nae, Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi ambaye aliwakilisha Wizara ya Afya akizungumza amesema mafunzo hayo yameshirikisha wataalamu kutoka sekta tofauti wakiwemo Polisi, madaktari wa mifugo, wataalamu wa majanga kutoka ofisi ya Waziri Mkuu, Ikulu, madaktari, wahudumu wa afya na taasisi nyingine za serikali.

“Sio kila janga wawe watu wa afya tu mstari wa mbele, hata watu kutoka sekta mbali mbali mchanganyiko inapotokea dharura ya majanga mahali popote wawe mstari wa mbele kudhibiti.”Amesema Janabi na kuongeza

“Mfano tu wakiwa wanaendelea na mafunzo kumetokea mlipuko Kagera, wapo waliotoka hapa wameenda na taarifa ya Wizara tunaelezwa kuwa ugonjwa umedhibitiwa kwa kiasi kikubwa.” Amesema

Amesema, mradi una lengo la kuendeleza kutumia mifumo na juhudi zilizopo na kuboresha zaidi utayari wa kukabiliana na matukio ya dharura na majanga.

Mradi huo unaojulikana kama “Flagship Initiative” utaisaidia nchi kuwa na mfumo sahihi wa kukabiliana na dharura na majanga kwa kuimarisha mpango kazi wa uwezo wa kujiandaa, kugundua na kukabiliana na dharura na majanga pamoja na kujizatiti.

Habari Zifananazo

Back to top button