Wataalamu Fifa kushuhudia michezo Umisseta

TABORA; Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Damas Ndumbaro, amesema kuwa mashindano ya michezo ya Shule za Msingi (Umitashumta) na yale ya sekondari (Umisseta) yanayofanyika nchini kila mwaka ni ya mfano duniani.

Dk Ndumbaro amesema hayo leo Juni 18, 2024 wakati akifungua rasmi mashindano ya Umoja wa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) yanayofanyika kitaifa mkoani Tabora.

Waziri Ndumbaro ameeleza kuwa ukubwa wa mashindano hayo umefanya wapokee pongezi kutoka  Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (Fifa), ambayo kwa mara ya kwanza imetuma wataalamu wake kufuatilia vipaji michezo ya mwaka huu.

“FIFA wametuma wawakilishi ambao ni wataalamu wa ufundi kushuhudia mashindano haya, wengine walikuwepo wakati wa Umitashumta na leo wanaingia wengine kuongeza nguvu kwa ajili ya Umisseta, huu ni ushahidi kuwa michezo hii ina thamani kubwa,” amesema Waziri Ndumbaro.

Ametaja maboresho makubwa ya mashindano ambayo yameendelea kufanyika kuwa ni kutokana na Serikali ya Awamu ya Sita kuendelea kuipa thamani michezo nchini hususani kwenye ngazi ya shule za msingi na sekondari.

“Juhudi hizi za Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan zinapaswa kuungwa mkono na wadau wengine wa michezo nchini, kwa sababu michezo ni ajira ambayo inatakiwa kuandaliwa kuanzia katika ngazi ya chini,” amesema.

Habari Zifananazo

Back to top button