Watafiti waja na chanzo ugonjwa wa kuvilia damu samaki

DAR ES SALAAM; TATIZO la ugonjwa wa kuvilia damu na vidonda kwa samaki wa kufugwa aina ya sato, sasa limepatiwa ufumbuzi baada ya kupatikana kwa chanjo.

Hilo limebainika wakati timu kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), ilipofanya ziara katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kilichopo Morogoro kujionea namna fedha za serikali kupitia tume hiyo zinavyotatua changamoto mbalimbali katika jamii.

Mtafiti wa chanjo hiyo kutoka SUA, Dk Alexander Mzula anasema chanjo hiyo imeshawanufaisha wakulima 96 kwenye Mikoa ya Ruvuma, Mwanza, na Arusha na inategemewa kunufaisha wafugaji wa sato kwenye mabwawa na vizimba zaidi ya 10,000.

Advertisement

“Chanjo hii itaongeza udhibiti wa ugonjwa huu ukilinganisha na utaratibu wa utunzaji wa mabwawa bila kutumia kinga yoyote kwa samaki sato,” anasema.

Anaeleza kuwa ametafiti chanjo hiyo kwa hatua ya pili kwa ufadhili wa  serikali kupitia Costech na ulilenga kujiridhisha na ufanisi wa chanjo hiyo ya kuzuia ugonjwa usababishwao na bakteria aina ya aeromonas hydrophila.

Ugonjwa huo wa kuvilia damu na vidonda ndio umekua tatizo kubwa ulimwenguni kote ambao unaweza kuua mpaka asilimia 100 ya samaki bwawani.

“Hapa kwetu Tanzania ugonjwa huu umeshajitokeza kwenye mikoa mbalimbali kama Ruvuma, Mbeya, Kilimanjaro, Iringa na Mwanza,” anasema.

Kuhusu samaki wa kufugwa Dk Mzula anasema huugua sana magonjwa mbalimbali ukilinganisha na samaki wasiofugwa.

Sababu kubwa ni uangalizi mdogo wa samaki hao kwenye mabwawa ikiwa ni pamoja na kujazana wengi ikilinganishwa na ukubwa wa bwawa, kutosafisha bwawa na kubadilisha maji, hali ambayo huwaweka samaki katika shinikizo la kupata magonjwa.

: Mtafiti wa chanjo hiyo kutoka SUA, Dk Alexander Mzula (aliyevaa koti) akiwa na watafiti kutoka Costech pamoja na watumishi wengine wa chuo hicho wakiangalia samaki kwenye bwawa lililojengwa. (Picha zote na Lucy Ngowi)

 

Upatikanaji wa chanjo hiyo ni jambo jema kwa kuwa mpaka sasa hakuna chanjo ya magonjwa ya samaki hapa nchini, hivyo basi hakuna mgongano wa kimaslahi uliopo na wazalishaji wa bidhaa hiyo.

Anasema Costech imefadhili utafiti huo wa ukamilishwaji wa chanjo ya ugonjwa huo wa samaki kupitia SUA ikishirikiana na Taasisi ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia.

Kuhusu chanjo hiyo anasema itauzwa kulingana na dozi na idadi ya vifaranga vya samaki watakaochanjwa.

Anasema chanjo hiyo ijulikanayo kama Aerovac ni rafiki kwa mazingira kutokana na jinsi ilivyotengenezwa kwani imetumia njia ya kufubaza nguvu ya bakteria hao aeromonas hydrophila kwa ajili ya kuhamasisha mwili wa sato mwenyewe kutengeneza kinga dhidi ya ugonjwa unaosababishwa na bakteria halisi.

Pia chanjo hiyo ni rafiki kwa mkulima kwa kuwa ni ya kuogesha samaki na mkulima atachanja vifaranga wa sato wengi kwa mara moja. Samaki wakiwa vifaranga huwekwa kwenye ujazo wa maji yaliyopimwa na dozi ya chanjo huwekwa kwenye maji hayo kwa dakika 45 wakiogelea.

“Utafiti unaonesha kuwa chanjo hii inaweza kukaa kwa muda wa miezi nane kwenye ubaridi wa kawaida wa jokofu bila kuharibika,” anasema.

Anasema hatua iliyofikiwa kwa chanjo hiyo ni kwamba, watafiti wameshatengeneza ombi la hakimiliki na kulituma mamlaka husika kwa ajili ya kulinda ubunifu huo.

Pia anasema utafiti huo uliochukua takribani miaka mitano matokeo yake yameanza kuonekana na itakaposajiliwa hivi karibuni itakuwa mkombozi kwa wafugaji wa sato nchini dhidi ya ugonjwa huo.

Anasema Costech iliwafadhili Sh milioni 120 kwa ajili ya kukamilisha chanjo hiyo, ili iongeze ufanisi na ikatumike moja kwa moja kwa wafugaji wao wa samaki.

“Hivyo majaribio yaliyofanyika mwishoni ni kupeleka kwa wakulima wa samaki kuweza kuona matokeo yake kwenye hali halisi ya mazingira ya hao wafugaji.

“Tunamshukuru Mungu chanjo imetoa matokeo mazuri sana na ufanisi wake umekuwa mkubwa kwa watu ambao tuliwafanyia majaribio,” anasema.

Maelezo yake ni kwamba wakulima hao 96 ndio waliotumiwa katika utafiti huo katika mikoa mitatu waliyofanya majaribio ambayo ni Ruvuma, Mwanza na Arusha.

“Na sasa tunategemea kuwa itanufaisha wakulima wengine zaidi ya 10,000 wa ufugaji wa sato wa kwenye mabwawa na vizimba,” anasema.

Anasema katika jamii kumekuwa na changamoto ya magonjwa hasa samaki kufa kutokana na ugonjwa huo wa kuvilia damu na vidonda hakukua na suluhisho maalum kwa sababu samaki hawawezi kutibiwa kwa kutumia dawa na hairuhusiwi kisheria.

Hivyo walifanya utafiti huo kwa kuwa suluhisho pekee ni ya chanjo ambayo inakubalika ulimwenguni katika magonjwa ya samaki.

Katika utafiti huo, anasema walichukua sampuli za samaki 820 kutoka kwenye mabwawa mbalimbali kwenye hiyo mikoa mitatu na walitoa maini, moyo na figo za samaki ili kuangalia wadudu wanaosababisha ugonjwa wa kuvilia damu pamoja na vidonda.

Katika kutafiti huko, walikuta asilimia 24.6 zilikuwa na vimelea wanaosababisha ugonjwa wa kuvilia damu pamoja na vidonda, ambao ukiingia kwenye bwawa unaweza ukasababisha vifo kwa asilimia 100.

Kwa hiyo kwa kutumia chanjo hiyo inawezekana kuchanja samaki wengi sana kwa mara moja ikilinganishwa na njia nyingine ambazo ni za kuchoma samaki kwa kutumia sindano.

“Jinsi ya kuchanja lazima uwe na bwawa au kontena maalum la kuwaogesha hao samaki kabla hujawapeleka kwenye mabwawa yao husika ambayo watakuwa huko na kwa sababu tuna chanja vifaranga samaki hawa huwa wanawekwa kwenye bwawa maalum ambapo uchanjaji huwa unategemea na dozi ya chanjo.

“Kwa mfano chanjo hii ni mililita 10 ambayo inachanja samaki wa kilogramu 100 kwenye maji ya lita 100. Maana yake kama unachanja samaki wa gramu 10 utahitaji samaki 10,000 kuwekwa kwenye hilo bwawa lenye ujazo wa maji lita 100,” anasema.

Kuhusu Chanjo hiyo, Ofisa Uvuvi Kituo cha Uwekezaji Viumbe hai, kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, mkoani Mbeya Luka Mgwera anakiri matokeo chanya ya chanjo hyo.

Anasema kabla ya kupatiwa chanjo hiyo kama sehemu ya majaribio samaki walipata maradhi kwa takribani asilimia 30 mpaka 40. Lakini baada ya chanjo.

“Hii chanjo ni nzuri sana nawasihi wakulima waendelee kuitumia. Baada ya kupata chanjo, anasema Mary Ismail kutoka Tangini wilaya Meru mkoani Arusha.

Timu ya Costech ipo kwenye ziara ya kutembelea tafiti na bunifu mbalimbali ambazo serikali imezifadhili kupitia tume hiyo, ili matokeo yake yaweze kutatua changamoto katika jamii.