Wataka mapambano malaria, dengue yawekwe pamoja

DAR ES SALAAM; Watafiti wametaka mapambano ya ugonjwa wa dengue na malaria yajumuishwe pamoja.

Kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa Machi 2024 katika Jarida la Kitabibu la Tanzania (TMJ), unaonesha umuhimu wa dengue kujumuishwa katika programu zilizopo kama vile za udhibiti wa malaria.

Watafiti wanasema njia hiyo inaweza kurahisisha upatikanaji wa rasilimali fedha za kuzuia magonjwa yote mawili kwa gharama nafuu na kuongeza uwezekano wa kuokoa maisha ya watu zaidi.

Mwaka 2019 zaidi ya watu 6,800 walipata maambukizi ya virusi vya dengue na vifo 13 vilirekodiwa wakati wa mlipuko wa mwisho wa dengue .

Mwaka mmoja baada ya mlipuko huo watafiti walichunguza jinsi Mpango wa Udhibiti wa Malaria unavyoweza kutumika pia kupambana na dengue.

SOMA:https://habarileo.co.tz/serikali-tumieni-kiwanda-cha-viuadudu-kibaha/

Jarida hilo linaeleza kuwa watafiti waligundua kuwa udhibiti wa dengue unaweza kujumuishwa kwenye programu za malaria, lakini walibaini changamoto kama utashi wa kisiasa kwa upande wa serikali, hofu kwamba njia hii inaweza kuongeza gharama za ziada na ikawa mzigo kwa wataalmu wa afya, pia kulikuwa na suala la vipaumbele tofauti vya wafadhili.

Dengue inachukuliwa kama miongoni mwa magonjwa wa Kitropiki yasiyopewa kipaumbele (NTDs) nchini, hii inamaanisha kuwa haina mpango maalum wa kitaifa.

“Tukifanya maamuzi ya kujumuisha udhibiti wa dengue katika programu za kudhibiti malaria, nchi inaweza kujenga mfumo wenye ufanisi zaidi na ufanisi wa kulinda afya ya umma,” amesema Katibu wa Afya wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Dorice Lyimo.

Lyimo ambaye pia ni mtafiti kiongozi wa utafiti huo, akishirikiana na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), walifanya mahojiano na maafisa 15 kutoka Mpango wa Kitaifa wa Kudhibiti Malaria (NMCP) na mpango wa Magonjwa ya Kitropiki Yasiyopewa kipaumbele (NTDs), waligundua kuna utayari miongoni mwa watumishi katika taasisi hizo.

“Wengi wao walionesha nia ya kubeba mzigo wa ziada wa dengue, na miundombinu iliyopo inaweza kutumika kwa magonjwa yote mawili,” anasema Lymo.

Kwa mujibu wa utafiti huo wadau waliohojiwa walionekana kukubaliana na njia hiyo ya udhibiti, “Mbu wa Aedes bado wapo katika jamii zetu na wanasambaza virusi vinavyosababisha homa ya dengue, hii inamaanisha kuwa hatua zetu dhidi ya mbu huyu wa dengue zinapaswa kuwa za muda mrefu,” anasema Lymo na kuongeza kuwa:

“Kwa matokeo haya, hoja yetu mahususi ni kwamba tufungamanishe udhibiti wa magonjwa haya yanayoenezwa na mbu nchini.

Hata hivyo watafiti walibaini kuna hofu juu ya gharama za uendeshaji miongoni mwa waliohojiwa na hili walilitilia maanani kama jambo la msingi na hivyo wanapendekeza kuwepo kwa ushirikiano baina ya idara mbalimbali za serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali, ili kutatua changamoto za gharama zinazoweza kujitokeza.

Mtafiti mwenza wa utafiti huo, Dk Nathanael Sirili, ambaye ni mhadhiri mwandamizi na mtafiti wa mifumo ya afya kutoka MUHAS, anasema kuwa ugonjwa wa dengue ukiendelea kuwekwa katika kundi la magonjwa yasiyopewa kipaumbele, utaendelea kutodhibitiwa inavyotakiwa na utazidi kuleta madhara.

Amesema kwa sababu za upungufu wa rasilimali watu na fedha kwenye sekta ya umma, Shirika la Afya Duniani (WHO), linapendekeza usimamizi jumuishi wa magonjwa kama hayo, ili kuziwezesha nchi kukabiliana vyema na changamoto zitokanazo na kudhibiti magonjwa yanayoenezwa na wadudu wakiwemo mbu.

“Dengue mara nyingi imewekwa katika kundi la magonjwa yasiyopewa kipaumbele kutokana na viwango vya chini vya vifo vinavyohusiana ugonjwa huo, hata hivyo mwanafamilia akipoteza maisha kutokana na dengue, inakuwa ni hasara ya asilimia 100 kwa familia,” amesema.

“Huu ugonjwa ukiwekwa kwenye udhibiti jumuishi na malaria, njia hii itaruhusu matumizi ya rasilimali chache lakini kutaleta matokeo makubwa zaidi,” amesema na kuongeza kuwa  hakuna haja ya kuwa na programu mbili ya dengue na malaria, kwani hiyo inamaanisha kuwa inabidi kutenga rasilimali kwa ajili ya dengue na nyingine kwa ajili ya malaria

Habari Zifananazo

Back to top button