Watakaochezea mifumo ya ukusanyaji mapato kukiona

WIZARA ya Fedha na Mipango imezindua Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma awamu ya sita itakayoimarisha mifumo ya ukusanyaji mapato na matumizi ya serikali, na itaendelea kuadhibu watendaji wenye nia mbovu za kucheza na mifumo hiyo.

Progrogramu hiyo pia itaangalia kwa undani ushirikishaji wanawake katika mipango, bajeti na vipaumbele vya serikali pamoja na masuala ya tabianchi.

Akizungumza katika uzinduzi wa Programu ya Maboresho hiyo jijini Dodoma jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Dk Saada Mkuya Salum alisema Programu ya Sita ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma (PFMRP VI) itatekelezwa nchini kwa miaka mitano kati ya 2022/23-2026/27.

Alisema tofauti na programu za maboresho zilizopita, hii itatumia wakaguzi wa ndani kubaini watendaji wanaocheza na mifumo ya kukusanya mapato hata kama serikali imeweka mifumo bora.

Katika kudhibiti watendaji wenye nia ovu ya kuchezea mifumo, itatumia wakaguzi wa ndani kubaini vitendo hivyo kabla ya wakaguzi wa nje hawajafika kukagua.

“Katika maboresho ya awamu ya sita masuala ya ushirikishaji wanawake na masuala ya tabianchi yameingizwa,” alisema Dk Mkuya.

Dk Mkuya alisema awamu hii ya sita imezinduliwa baada ya kufanya tathmini ya awamu ya tano (PEFA), na wamebaini serikali imefanya vizuri katika kusimamia mapato na matumizi ya fedha za umma, lakini bado kuna changamoto chache katika makusanyo na matumizi.

Changamoto hizo zimekuwa zikipungua awamu kwa awamu kutokana na mkakati wa serikali wa kuwajengea uwezo wa vifaa na kitaaluma watendaji na taasisi kuangalia mapato na matumizi ya serikali ikiwamo ofisi za Mkaguzi wa Hesabu za Serikali Bara na Zanzibar.

Aidha, serikali pia imejengea uwezo taasisi za kudhibiti na kupambana na rushwa Tanzania na Zanzibar ili kuchunguza na kubaini vitendo vya rushwa kuhakikisha mapato na matumizi ya serikali yanatumika vizuri.

Pia imewezesha taasisi kama Bunge na Baraza la Wawakilishi kuhakikisha wanahoji na kuishauri serikali kuhusu mapato na matumizi ya fedha za umma.

Hiyo, Dk Mkuya alisema awamu hii inalenga kuendelea na mageuzi katika kukusanya mapato na kuangalia matumizi kwa kuwezesha zaidi wakaguzi wa ndani.

Pia, inalenga kuboresha ukusanyaji na usimamizi wa mapato na matumizi katika ngazi za halmashauri ambako kama kukisimamiwa vizuri kuna mapato mengi.

Dk Mkuya alipongeza mchango wa ushiriki wa wadau wa maendeleo katika kutekeleza programu zilizopita na mkakati wa kuendelea kusaidia programu ya sita.

Katika maboresho hayo, wadau wa maendeleo hasa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake wameshauri suala la wanawake lipewe kipaumbele.

Habari Zifananazo

Back to top button