VIJANA kutoka kaya maskini wanaoishi katika mazingira magumu nchini, wameshauriwa kuchangamkia fursa za mafunzo ya kukuza na kuendeleza ujuzi yanayotelewa na serikali kupitia vituo mbalimbali vya mafunzo ya elimu ya ufundi na ufundi Stadi.
Ushauri huo umetolewa Kisiwani Unguja na Mkurugenzi wa Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Waziri Salum alipokuwa katika ziara ya siku mbili ya kutembelea wanafunzi kutoka kaya maskini wanaosoma mafunzo ya ujuzi kupita mpango wa ufadhili kwa vijana kutoka kaya maskini na wanaoishi katika mazingira magumu.
Amesema serikali inawatambua na kuwathamini vijana hao na iko tayari kuwasidia waweze kujikwamua kiuchumi na kujihusisha katika shughuli mbalimbali za ujasiriamali na uzalishaji mali, aidha kwa kujiajiri wenyewe au kuajiriwa ili wajipatie kipato.
Amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ilizindua rasmi Mpango wa Ufadhili kwa Vijana kutoka Kaya Maskini na wanaoishi katika mazingira magumu Desemba mwaka jana kwa lengo la kutoa mafunzo ya ujuzi kwa vijana 600 kutoka kaya maskini katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Amesema amefarijika kuona vijana hao wanavyojituma na kuweka bidii kwenye masomo yao, hivyo kuwaasa wasikate tamaa ya kupambania kile wanachokiamini, kwani watazifikia ndoto zao za kujikwamua kiuchumi na kujipatia kipato.
Awali Mkurugenzi Waziri amesema, wakati mafunzo hayo yanazinduliwa hawakujua kama wangepata wanafunzi wa makundi gani, ila baada ya mafunzo kuanza vijana walemavu na wenye mahitaji maalum ni miongoni mwa waliopata fursa ya kusoma mafunzo hayo ya ujuzi kupitia mpango huo wa kaya maskini.
“Fursa bado zipo na Serikali bado inawakumbuka, mkimalimaliza masomo jiungeni kwenye vikundi na mjisajili mfanye kazi kwa umoja ili muweze kuzifikia fursa nyingi zaidi, “amesema Waziri.